Wednesday, December 5, 2012

Matokeo ya maoni juu ya katiba mpya shehia ya Dimani asubuhi ya leo.



Wananchi wa Dimani wakitoa maoni yao juu ya katba mpya
Wananchi wa Dimani wakitoa maoni yao juu ya katba mpya
Matokeo ya maoni juu ya katiba mpya shehia ya Dimani wananchi waliotaka Zanzibar huru ikufuatiwa na muungano wa mkataba kati ya Zanzibar na Tanganyika ni 25.
Na wananchi waliotaka muungano huu uliopo uendelee kama ulivo ni87.

MJI MKONGWE UNAHITAJI KUTUPIWA MACHO


Salim Said Salim Mwandishi wa habari mkongwe Zanzibar
Salim Said Salim Mwandishi wa habari mkongwe Zanzibar
MWISHONI mwa wiki sehemu ya nyuma ya jengo maarufu na la kihistoria la Beit el Ajaib (Nyumba ya Ajabu) liliopo Forodhani, Mjini Unguja, liliporomoka. Kwa bahati njema hayakutokea maafa makubwa, lakini kuanguka kwa majumba haya katika sehemu mbalimbali za Mji Mkongwe ni hasara kubwa kwa historia ya mji wa Zanzibar.
Tukio hili la kuporomoka kwa jengo la Beit el Ajaib, lililopo pembezoni mwa Ngome Kongwe iliyojengwa na watawala wa Kireno, ni kuendelea kuporomoka majengo ya zamani, baadhi yao yalijengwa takribani miaka 200 iliyopita katika Mji Mkongwe.
Jengo hili la ghorofa tatu, kila moja likiwa na urefu wa zaidi ya futi 40 ambalo linatazama na bandari ya Zanzibar, lilijengwa na Sultan Seyyid Barghash bin Said (1880-88), ni la ina yake na hakuna linalofanana nalo katika Afrika ya Mashariki.
Kwa muda mrefu sasa jengo hili maarufu duniani kote, kama yalivyo mengine mengi ya zamani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, yameonekana kuchakaa na kuhitaji matengenezo ya haraka.
Baadhi yamekuwa yakiporomoka moja baada ya jingine, hasa wakati wa mvua za masika au vuli na hata kusababisha maafa na hasara kubwa.
Kwa kweli hali iliyojitokeza ni ya kusikitisha. Hata hivyo, baadhi ya majumba haya, yamefanyiwa ukarabati mkubwa kwa misaada kutoka taasisi za Umoja wa Mataifa na nyingine za kimataifa. Miongoni mwao ni iliyokuwa nyumba ya sultani, zahanati ya jamii ya Ismalia na nyingine nyingi.
Majengo yaliyofanyiwa ukarabati sasa yanapendeza na kuwa vivutio kwa watalii, lakini toka kufanyiwa ukarabati huo zaidi ya miaka 15 iliyopita, hakuna juhudi za kuyatunza na labda yanangojewa yachakae na kutafutiwa misaada ya kuyakarabati kutoka nje.
Majumba haya ya zamani na njia nyembamba za sehemu ambazo yapo, ndiyo yaliyosababisha Mji Mkongwe wa Zanzibar kuvutia utalii na kutangazwa kama urithi wa dunia.
Lakini jambo la kusikitisha ni kuona yametupwa na serikali. Wakati umefika kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wananchi wa Visiwani kwa jumla kutambua kuwa Mji Mkongwe ni urithi unaotaka kuenziwa na kutoruhusu kupotea.
Sio vibaya kutarajia nchi za nje na mashirika ya kimataifa kusaidia kutunza majengo haya ya kihistoria, lakini ni aibu na fedheha kuona wao ndio wanaotarajiwa kuyashughulikia.
Hii ni historia ya Zanzibar na ni watu wake ndio wanaowajibika kwanza kuyatunza na wageni kusaidia tu.
Kwa muda mrefu sasa nchi yetu imebweteka kwa kutegemea misaada hata ya kutengeneza bustani au ujenzi wa vyoo vya shule. Tumejenga utamaduni wa kuona hiyo ni kazi ya wageni na sio yetu, kama vile historia ya Zanzibar haina uhusiano na watu wake.
Lazima kwa serikali na wananchi kubadilika na kuyaona majengo haya ya kale, hasa yale yenye historia ya kuvutia kama Beit el Ajaib, yanatunzwa na kushughulikiwa ipasavyo.
Kichekesho kingine ni kwamba panapotokea taasisi ya Visiwani kutafuta fedha za kukarabati majengo ya zamani, kama lilivyofanya Baraza la Biashara, wamiliki wa viwanda na wakulima kwa jumba maarufu la mvumbuzi wa kiingereza, David Livingstone, baadhi ya viongozi wa serikali huja juu kutaka majengo haya yakabidhiwe serikali.
Hivyo serikali ilikuwa wapi wakati majengo haya yalipokuwa karibu kuporomoka? Huu sio mwenendo mzuri hata kidogo na unawakatisha tamaa Wazanzibari wanaoipenda nchi yao na wenye nia njema ya kusaidia kuyatunza majengo haya ya zamani.
Mwenendo huu hauna maelezo yoyote yale isipokuwa ni kielelezo cha roho mbovu kwa baadhi ya watu waliopo madarakani.
Tuache tabia hii inayowavunja moyo wananchi kwani kuyakakarabati na kuyatumia majengo hayo haina maana kwamba wameyataifisha kwani yanabakia kuwa mali ya serikali na wao kama wananchi ni sehemu ya serikali.
Kwa sasa tunapaswa kubadilika na kuwa na mpango maalumu wa kutenga vifungu vya fedha katika bajeti zetu za matumizi ya serikali ya kila mwaka kwa ajili ya kuyahudumia majengo haya ya kihistoria tuliyorithi kutoka kwa wazazi wetu.
Tukumbuke kuwa watalii wengi na wana-historia hufika Zanzibar kuyaangalia majengo haya ya kihistoria, lakini tukiyaruhusu kuporomoka hao watalii watakuja Zanzibar kufanya nini?
Wakati umefika na kwa kweli tumechelewa, kwa serikali kuhakikisha kuwa katika bajeti yake ya matumizi ya kila mwaka panatengwa fungu maalumu la kuyashughulikia majengo ya zamani, hasa yale ya kihistoria.
Kama tunaweza kutafuta fedha kujenga majumba mapya ya wizara za serikali na kuonekana kuwepo mashindano ya kufanya hivyo, kwanini tushindwe kutafuta fedha za kuilinda historia yetu? Ni kweli haiwezekani kuyakakarabi yote kwa wakati mmoja, lakini inawezekana kuifanya kazi hii kwa uwamu.
Kinachohitajika ni kuwepo mpango mzuri badala ya sehemu kubwa ya mapato ya serikali kutumika kwa safari za viongozi zisokwisha na kujinunulia magari ya fahari kwa viongozi na watumishi wa idara na taasisi za serikali.
Haya yanafanyika huku tukijigamba kwamba ati tunafanya kila juhudi za kupunguza umasikini unaowakabili watu wetu. Huku ni kujidanganya na wananchi wanajiuliza masuala mengi na kukosa majibu.
Sio vizuri kujikita kwa mambo ya fahari na anasa na kuipa mgongo historia yetu. Vizazi vijavyo havitatusamehe kama tutayatelekeza majengo haya na kupotea na watu kubaki kuhadithia habari za majengo haya wakati yakiwa yameshatoweka. Hawatatusamehe hata kidogo kwa kushindwa kuwarithisha historia hii tuliorithi kutoka kwa wazazi waliotutangulia mbele ya haki.
Watajiuliza hawa wazee wetu walikuwa watu wa aina gani na wakati huo hatutakuwepo katika dunia hii kujitetea.
Tuchukuwe juhudi sasa ya kuhifadhi maeneo muhimu ya historia Unguja na Pemba ili historia isije kutuumbua kwa kuipoteza sehemu muhimu ya historia ya Zanzibar na watu wake.

Sunday, December 2, 2012

WAHAMIAJI WAPO HATARINI ZAIDI KUAMBUKIZWA UKIMWI

Wahamiaji wako hatarini zaidi kuambukizwa Ukimwi: IOM

Kusikiliza / Hamishia
Shirika la kimataifa la Uhamiaji, IOM limesema wahamiaji wanaathirika zaidi na virusi vya ukimwi na Ukimwi hususan katika nchi zenye vipato vya juu.
IOM inasema kuwa ripoti ya mwaka huu ya UNAIDS inaonyesha kuwa kwa mara kwanza katika historia ya Ukimwi, maambukizi mapya ya ugonjwa huo katika nchi zilizokuwa na mzigo mkubwa wa maambukizi hayo yanapungua, lakini bado kuna changamoto.
Ripoti hiyo inatoa mfano wa nchi zenye vipato vya juu kama zile za Amerika Kaskazini na Ulaya ambako inasema idadi ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi imeongezeka katika kipindi cha miaka Kumi iliyopita.
Imesema wahamiaji na watu wanaohamahama wako hatarini zaidi kuambukizwa virusi hivyo kwa sababu mipango mingi ya afya huwaengua mara kwa mara na hata hawawezi kupata huduma za afya. Jumbe Omari Jumbe ni msemaji wa IOM
((SAUTI YA JUMBE OMARI JUMBE)

ZANZIBAR HEROES WAPIGWA 2-0


Zanzibar Heroes yalala kwa Malawi 2 – 0, yatinga robo fainali CECAFA

Wachezaji wa Zanzibar Heroes

Wachezaji wa Zanzibar Heroes
Timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, leo hii imefungwa 2-0 na timu ya taifa ya Malawi katika mchezo wa mwisho wa kundi C katika mchezo uliopigwa katika uwanja wa Wankulukuku. Magoli ya Malawi yalifungwa mapema ambapo Ndaziona Tchasalia aliweka kimioni bao la kwanza dakika ya 3 baada ya mchezo kuanza huku goli la pili likifungwa na Chuikepo Msowoya katika dakika ya 6 ya mchezo huo.
Licha ya kujaribu kusawazisha, Zanzibar Heroes  ilijikuta ikikabiliana na ukuta mgumu wa timu ya Malawi ambayo pia imefanikiwa kuingia katika Robo fainali kwa kumaliza na pointi sita.
Hata hivyo, Zanzibar Heroes nayo imeweza kufuzu kuingia robo fainali kutokana na kuwa “best loser” kwa kuweza kupata pointi nne katika mechi zake mbili za awali dhidi ya Eritrea na Rwanda.
Itapambana na Burundi siku ya Jumatatu saa 10.00 jioni katika mchezo unaotarajiwa kutoa upinzani mkali kwani Burundi haijapoteza kupoteza hata mchezo mmoja katika kundi lake huku Zanzibar ikijaribu kukumbuka historia yake ya kuweza kulinyakua kombe la CECAFA mwaka 1995 katika nchi ya Uganda.

Saturday, December 1, 2012

USHAIRI

Kulikumba Jini

Kulikumba Jini
Utumwa naliopewa, nende kwa jini nifike
Hamshike sawasawa, nimfunge afungike
Ashindwe jipapatuwa, chupani nimfundike
Kisha nende panganikwe, silisili kumtia
Na vifaa nikapewa, na nyenzo za uhakika
Makombe hazinguliwa, ya kunywa na ya kupaka
Na kafara hasomewa, na hirizi hajivika
Alipo nikamfika, lengo kwenda mchukuwa
Halikuta kubwa jini, lisilo mfano wake
Tangu juu hadi chini, sioni khatima yake
Katikati msituni, ‘meketi kitini pake
Bali nisitetemeke, nili nikijiamini Read the rest of this entry

Ningekuwa Sikupendi

Ningekuwa Sikupendi
Ningekuwa Sikutaki
Ningekuwa sikutaki, sege nawe ‘singekaa
Nisingefanya dhihaki, usoni ningekwambia
‘Singejipatisha dhiki, wala ‘singeng’ang’ania
Lakini n’nabakia, sababu nakuashiki
‘Ngekuwa sikuhitaji, kale ningeshakwachia
‘Singekufaya mkwiji, nendapo nakuchukua
Hawa hayapiti maji, bilawe kukuwazia
Sababu ya yote haya, wewe kwangu kama taji
Ningekuwa sikupendi, siri ‘singekufanyia
‘Singeupiga umundi, na boso na tarazia
Kusema halinishindi, wazi nikakuwekea
Lakini nawe wajua, mapenzi hayana fundi
Read the rest of this entry

U Wapi Ewe Furaha?

U Wapi Ewe Furaha?
Ninakujua Furaha hu mja wa kusalia
Hu mja unayekaa daima ukabakia
Huja mara ukangia na mara ukapotea
Lakini hebu rejea! Read the rest of this entry

JENGO LA BEIT- EL- AJAIB LAPOROMOKA ZANZIBAR


Beit el Ajab yaporomoka

Jengo la Beit-el-Ajaib likiwa limeanza kuporomoka upande mmoja.

Jengo la Beit-el-Ajaib likiwa limeanza kuporomoka upande mmoja.
Jengo maarufu la kihistoria Zanzibar, Beit-el-Ajab (Nyumba ya Ajabu) limeporomoka usiku wa tarehe 1 Disemba 2012. Akizungumzia tukio hilo, mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe ambako ndiko liliko jengo hilo, Ismail Jussa, alikuwa na haya ya kusema kupitia mtandao wa Facebook: “Aibu iliyoje leo kufikia Beit-el-Ajaib kuanguka baada ya Serikali kupuuza hatua zote za kuwazindua kuwa jengo hilo liko katika hali mbaya. Katika kikao cha Bajeti cha Baraza la Wawakilishi cha mwezi Juni/Julai 2011 na 2012 nilizungumzia suala la uwezekano wa majengo haya ya kihistoria kuanguka kutokana na kutotunzwa au kufanyiwa matengenezo.
“Nikaandika na swali maalum kuhoji matengenezo ya majengo hayo hasa baada ya mradi wa MACEMP unaofadhiliwa na nchi wahisani na mashirika ya kimataifa kuwa na fungu la matengenezo la majengo ya Kasri (Palace) na Beit-el-Ajaib. Kama kawaida ya majibu ya Serikali, tuliambiwa, ‘Tusiwe na wasiwasi’. Nikatahadharisha kuwa binafsi nimeyatembelea majengo hayo mawili kuona pamefanyika matengenezo gani kutokana na fedha zilizotengwa, na kuona hapana matengenezo ya maana. Nikajibiwa, ‘Tutafuatilia’. Sasa leo hii turathi ya kitaifa (national heritage) ambayo ni jengo la kwanza refu katika Afrika Mashariki, la kwanza kuwa na umeme na la kwanza kuwa na lifti kiasi cha kuitwa Jumba la Ajabu (House of Wonders) limeanguka kwa uzembe wa Serikali. Shame on them!”
Naye mwandishi wa habari wa siku nyingi visiwani Zanzibar, Ally Saleh alikuwa na haya ya kuandika kulilia jengo hilo ambalo limekuwa alama ya Zanzibar kwa karne na karne:

POLISI AJERUHIWA ZNZ

Polisi ajeruhiwa kwa mapanga Zanzibar

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa
Watu wasiojulikana wamemvamia askari polisi mmoja na kumjeruhi kwa mapanga, mnamo majira ya saa 10:00 alasiri katika huko Mboriborini kando kidogo ya mji wa Zanzibar. Imeripotiwa kwamba kundi hilo la watu lilimvamia askari huyo anayejulikana kwa jina la Othman Juma na kufanikiwa pia kuchukua pesa alizokuwa nazo ingawa haijajulikana ni kiasi gani mpaka sasa. Hatua za kumpatia matibabu askari huyo zinaendelea vizuri katika hospitali ya Al Rahma, Kilimani Unguja.