Chama
Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) vimeshutumiana vikali
kuhusiana na kuvunjika kwa mikutano miwili ya kutoa maoni ya katiba
Visiwani Zanzibar juzi. CCM wamesema vurugu zinazotokea katika vituo vya
kutoa maoni ya katiba zinaratibiwa na CUF na kutaka Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kuchukua hatua dhidi ya watu walioamua kuvunja sheria. Tamko
hilo lilitolewa jana na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi
na Uenezi ya CCM Zanzibar, Issa Haji Gavu, alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari mjini Zanzibar. “Haya yanayofanyika sasa na kutokea
ni matendo maovu, ni uhalifu na zaidi yakitaka kuturudisha tena katika
zama nyeusi za mivutano, malumbano na kujenga upya uhasama,” alisema
Gavu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar.
Alisema CUF imekuwa ikisafirisha wafuasi wake wanaotetea Muungano wa
mkataba katika magari kwenda kutoa maoni katika maeneo wasiyoishi na
kusababisha vurugu kati yao na wakazi halali katika maeneo hayo. Gavu
alisema watu wanaosafirishwa siyo wenye ulemavu wa viungo, lakini
wanalazimika kusafirishwa kwa magari kwa kuwa ni wageni katika maeneo
wanayokwenda kutoa maoni. “Matukio haya kwa sehemu kubwa yana lengo la
kuleta mmomonyoko wa kutovumiliana na kutostahamiliana kulikoanza
kustawi na hivyo kujenga wasiwasi na hofu,” alisema Gavu. Hata hivyo,
alisema kwamba pamoja na wanachama wa CCM kuzomewa wanapotoa maoni
kuhusu kuendelea kwa mfumo wa Muungano wa serikali mbili, CCM itaendelea
kutetea mfumo huo kwa nguvu zake zote kwa vile ndiyo msingi wa ilani
yake ya uchanguzi ya mwaka 2010-2015. “Tunaamini kuwa maoni na mawazo ya
kila mwananchi kwa ajili ya uundwaji wa katiba mpya ni sehemu ya
utekelezaji wa misingi ya demokrasia na mtu yeyote hapaswi kuwekewa
mipaka au ukomo wa kutoa mawazo yake,” alisema. Alisema kuwa CUF imekuwa
ikipandikiza watoa maoni mamluki ambao tayari wametoa maoni katika
majimbo yao baada ya kuona wananchi wanaotaka mfumo wa Muungano wa
serikali mbili ni wengi katika shehia mbalimbali. “Ili uonekane bingwa,
mwenye uchungu na Zanzibar, mzalendo wa kweli na mwana mageuzi makini,
unalazimishwa utoe maoni yanayopendekeza mfumo mpya wa Muungano wa
mkataba na hutakiwi utoe maoni ya serikali mbili, huu ni uvunjaji wa
misingi ya demokrasia,” alisema Gavu. CUF YAJIBU Mkurugenzi wa Haki za
Binadamu, Habari na Uenezi wa CUF, Salum Bimani, alikanusha chama hicho
kuhusishwa na matukio ya vurugu hizo na kusisitiza kwamba zinafanywa na
wabunge na wawakilishi wa CCM. Alisema viongozi hao wamekuwa wakikusanya
watu katika matawi ya CCM na kuwapeleka kutoa maoni ya Katiba kwa
kutumia utaratibu maalum wa kupangwa mwanzo na kuwanyima haki watu
wanaoonekana kuwa ni wafuasi wa vyama vya upinzani. Aliwataka baadhi ya
wabunge na wawakilishi wa CCM (majina tunayahifadhi) kuwa wamekuwa
wakifanya kazi ya kupeleka watu kwenda kutoa maoni yanayoinga mkono ya
Muungano wa serikali mbili. Bimani alidai kuwa pamoja na Tume hiyo
kuongozwa na wanasiasa wakongwe na watu wanaoheshimika katika jamii
wakiwamo Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba; Jaji Mkuu Mstaafu,
Augustino Ramadhan na Waziri Mkuu Mstaafu, Salim Ahmed Salim, lakini
kazi imewashinda kutokana na majukumu ya tume kutekwa na viongozi wa CCM
Zanzibar. Alisema wananchi wamekuwa wakikusanywa na kupewa posho na
kupikiwa pilau mambo ambayo yalitakiwa kukemewa na Tume na kuchukua
hatua kali dhidi ya watu na viongozi wanaofanya vitendo hivyo. KAULI YA
WARIOBA Kwa upande wake Warioba, alijibu madai ya Bimani na kusema kuwa
vyama vya siasa vikae pembeni na kuwaacha wananchi watoe maoni yao bila
kuingiliwa wala kushinikizwa. Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu
jana, Jaji Warioba alisema wao wanafanya kazi ya kuchukua maoni ya
wananchi na kwamba hawasikilizi vyama vya siasa vinasema nini. “Sisi
bado tunaendelea na kuchukua maoni ya wananchi ili waweze kupata katiba
mpya na wala hatusikilizi na kuangalia vurugu za vyama vya siasa,”
alisema na kuongeza: “Tunavitaka vikae pembeni na kuwaacha wananchi.”
Alisema mchakato wa kukusanya maoni unahusu wananchi na kwamba hawataki
kufanyi kazi ya kulumbana na vyama vya siasa na kuacha kazi waliyopewa.
POLISI WAZUNGUMZA Jeshi la Polisi Zanzibar limesema mabishano makali
yaliyoibuka katika vituo vya kutoa maoni ya Katiba ndiyo chanzo cha
mikutano miwili kuvunjika. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi,
Unguja, alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumzia vurugu za juzi
zilizosababisha kuvunjika kwa mikutano miwili katika majimbo ya Mpendae
na Magomeni. Alisema mabishano hayo yamekuwa yakitokana na kundi moja la
wananchi kulalamika kuwapo watu wanaojitokeza kutoa maoni wakati siyo
wakazi halali katika maeneo ambayo mikutano hiyo inafanyika. Hata hivyo,
alisema jeshi hilo tayari limechukua hatua mbalimbali kuhakikisha tume
hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake ikiwamo kuimarisha ulinzi.
Kamanda huyo alisema kuwa hadi jana hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa.
No comments:
Post a Comment