Wednesday, January 9, 2013

Maalim Seif akemea baadhi ya Wazazi kuwanyima watoto fursa ya Elimu

Rate This

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikata utepe kuashiria ufunguzi wa jengo la madarasa manne la skuli la Mbuyutende jimbo la Matemwe. Wa pili kulia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamuhuna.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amekemea tabia ya baadhi ya wazazi na walezi kuwanyima fursa za kielimu watoto wa kike, hatua ambayo inadumaza maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Amesema moja kati ya malengo makuu ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ni kuondoa ubaguzi wa aina zote, sambamba na kuwapatia elimu watoto wote bila ya kuwepo ubaguzi wa kipato au jinsia.
Maalim Seif ameeleza hayo leo baada ya kufungua jengo la madarasa manne la skuli ya Mbuyutende jimbo la Matemwe, ikiwa ni katika shamrashamra za maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema elimu ndio msingi wa maendeleo kwa watoto, hivyo wazazi wanapaswa kuwapatia elimu watoto wao, ili kuhakikisha kuwa wanawajengea mazingira bora ya maisha yao ya baadae.
Sambamba na hilo Maalim Seif ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuangalia uwezekano wa kuifanyia marekebisho  mitaala yake ya elimu, ili iendane na wakati na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
“Wapo vijana wengi wamemaliza hadi vyuo vikuu lakini hawana ajira, kwa hivyo mitaala yetu hii lazima iwaandae vijana waweze kujiari wanapohitimu masomo yao”, alifahamisha Maalim Seif.
Kuhusu upungufu wa walimu katika skuli za vijijini Maalim Seif amesema tatizo hilo linachangiwa na ukosefu wa nyumba za walimu, na kutoa wito kwa Wizara ya Elimu kushirikiana na serikali ya Mkoa huo kutafuta nyumba za walimu ili kuondosha tatizo hilo.
“Ukosefu wa nyumba za walimu ndio tatizo la msingi la upungufu wa walimu katika skuli za vijijini, kwa hivyo Wizara ya Elimu shirikianeni kwa karibu na Mkoa pamoja na Halmashauri kutafuta nyumba ijapo za kukodi, ili walimu wanaotoka mbali wapate mahali pazuri pa kuishi”, aliagiza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akijizungumza katika hafla ya ufunguzi wa jengo jipya  la madarasa manne la skuli ya Mbuyutende jimbo la Matemwe.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akijizungumza katika hafla ya ufunguzi wa jengo jipya la madarasa manne la skuli ya Mbuyutende jimbo la Matemwe.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Ali Juma Shamuhuna ameahidi kukamilisha upatikanaji wa madawati katika skuli hiyo, ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira bora.
Katika risala ya wananchi wa kijiji cha Mbuyutende iliyosomwa na nd. Makame Juma, wananchi hao wamesema licha ya mafanikio waliyoyapata katika kijiji hicho, bado wanakabiliwa na matatizo kadhaa yakiwemo ukosefu wa maji safi na salama, umeme na barabara.
Katika hafla hiyo jumla ya shilingi milioni 11 na laki nne zimechangwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo jipya la skuli hiyo ambapo Maalim Seif ameahidi kuchangia shilingi milioni tano.
Wanafunzi wa skuli ya Mbuyutende jimbo la Matemwe wakimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika hafla ya ufunguzi wa jengo jipya la skuli hiyo, licha ya kuwepo na jua kali wakati huo.

No comments:

Post a Comment