Thursday, January 10, 2013

Nyumba 19 zachomwa moto kwa makusudi

Nyumba ikiteketea kwa moto.



 
 
 
 
 
 
Rate This

NYUMBA 19  ambazo idadi ya wakazi wake haikujulikana mara moja zimeteketea kwa moto unaodaiwa kuwashwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa akishirikiana na polisi wa Kituo ch Staki Shari jijini Dar es Salaam.
Nyumba hizo zilijengwa katika Mtaa wa Vikongoro, Kata ya Chanika  Wilaya ya Ilala katika eneo ambalo linadaiwa kuwa na mgogoro.
Akisimulia tukio hilo, mkazi wa kitongoji hicho, aliyejitambulisha kwa jina la Yusuph Kondo (80) alisema mchana wa jana alimwona Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa  akiwa na  kidumu cha mafuta na kwamba alielekea kwenye nyumba ya Zaituni Mguguli na mara baada ya kufika eneo hilo aliona moto ukiunguza nyumba.
Naye mtoto wa Zaituni aitwaye Ajuaye Twaha(10), alisema walifika mwenyekiti akiwa na askari na kumwamuru atoke nje  na kwamba alimuona askari akimwagia mafuta na kuwasha moto.
Akizungumza kwa masikitiko, Zaituni alisema samani za ndani, magodoro na Sh 900,000 alizopewa  na mtoto wake wa kwanza ili kumlipia ada mdogo wake ziliungua ndani ya nyumba hiyo.
Miongoni mwa wakazi waliopata hasara kutokana na  tukio la kuungua nyumba zao, ni Fikiri Hassan, Zuberi Kiiba, Asha Abdallah,  na Issa Salehe.
Ofisa Mtendaji wa mtaa huo, Ali Kambi, alipoulizwa juu ya tukio hilo alikiri  na kwamba lilitokana na mgogoro  wa ardhi.
Alisema waliochomewa nyumba wote walivamia eneo la mtu anayeitwa Nicolaus Malose aliyemilikishwa na kijiji tangu 2011.
Hata hivyo waathirika wa tukio hilo walisema eneo hilo ni lao tangu mwaka 1985.
Mkuu wa Kanda ya Kipolisi   Ilala, Marietha Minongi Komba alipoulizwa jana kuhusu  tukio hilo alisema hakuwa na  taarifa  za kuungua kwa nyumba na kwamba siku ya jana alizungumza  na Mkuu wa  Kituo cha Polisi Ukonga mara saba, lakini hakupata taarifa zozote.

Kuzuiliwa kwa Hudur na Al-Shabaab kunawaadhibu wakaazi

Kutoka vikosi shirika vilipoilazimisha al-Shabaab kuachia udhibiti wa Hudur mwezi Machi 2012, kikundi hicho cha wanamgambo kimeamua kuzuia kuingia na kutoka katika jiji hilo na kuondoa usambazaji wa vyakula muhimu.
  • Mwanamke akitembea kuelekea hospitali huko Hudur mwezi Juni 2012. Jiji hilo limekuwa chini ya vizuizi vya al-Shabaab kwa takribani mwaka mmoja. [William Davies/AFP] Mwanamke akitembea kuelekea hospitali huko Hudur mwezi Juni 2012. Jiji hilo limekuwa chini ya vizuizi vya al-Shabaab kwa takribani mwaka mmoja. [William Davies/AFP]
Adan Abdalla Ahmed, mwenye umri wa miaka 52, ambaye anauza nguo huko Hudur, alisema al-Shabaab inajaribu kuleta mvutano baina ya wakaazi na serikali ya Somalia kwa kufanya maisha kuwa magumu zaidi pamoja na kufanya bei za vyakula kuwa juu sana.
Wanamgambo wa Al-Shabaab ambao wanadhibiti vijiji na miji kuzunguka Hudur wamezuia magari ya vyakula na bidhaa yanayotokea Mogadishu kutokwenda zaidi ya wilaya ya Abal, kilometa 20 mashariki mwa Hudur, mji mkuu wa mkoa wa Bakol.
"Wapiganaji wa al-Shabaab wamejipanga kwenye barabara zote zinazoingia mjini na wamesimamisha kila kinachoingia humo," Ahmed aliiambia Sabahi, akiongeza kwamba hata wafugaji waliokuwa wakileta maziwa Hudur wamezuiwa kuingia.
"Wanamgambo hao wanamtishia yeyote anayekwenda au kutoka katika mji na kuwaambia watauawa kama watakamatwa wakija Hudur tena," alisema.
Warder Ahmed Abdi, mwenye umri wa miaka 30, anayeleta chakula Hudur kwa kutumia punda kutoka maeneo ya jirani, alisema wafanyabiashara wanaoleta chakula katika mji wanahatarisha maisha yao kila wakati wanapoingia Hudur. Alisema wafanyabiashara wanaishia kutumia njia ndefu ili kukwepa vizuizi vya barabarani vya al-Shabaab.
"Tunapoondoka wilaya ya Abal, hatuwezi kutumia njia ya moja kwa moja [kwenda Hudur] na tunalazimika kuwakwepa al-Shabaab na kujificha," Abdi aliiambia Sabahi. "Kama wapiganaji wa al-Shabaab watatuona, watatudhuru na kuchoma bidhaa zetu. Watatutendea vibaya na kutishia kutuua kama tutajaribu kupeleka bidhaa tena Hudur."

Wanawake na watoto ndio wanaoathirika zaidi

Halima Nur, mkazi wa Hudur mwenye umri wa miaka 35, alisema al-Shabaab inasababisha madhara zaidi kwa wanawake na watoto wa Hudur.
"Nilikuwa ninamiliki duka dogo katika mji ambako niliuza chai kwa ajili ya kutafuta riziki ya watoto wangu. Hilo limekuwa gumu sana, kwani kila kitu kimekuwa ghali sana. Sijui cha kufanya kwa sababu mji mzima umefungwa na hakuna yeyote anayeweza kutoka."
"Haya sio maisha," alisema Nur, mjane na mtoa huduma pekee kwa watoto wake watatu.
Mkuu wa Wilaya Mohamed Moalin Ahmed alisema utawala wake unajua shida al-Shabaab inayowaletea wakaazi wa Hudur na kwamba wanashughulikia kurejesha hali ya kawaida na kulikomboa eneo hilo "hivi karibuni".
"Chini ya utawala wangu, tumefundisha kikosi cha kijeshi chenye takriban wanajeshi 800 kwa msaada wa jeshi la Ethiopia katika eneo la Bakol," alisema Ahmed. "Wanajeshi hao sasa wako tayari kuchukua nafasi katika ukombozi wa maeneo yaliyoshikiliwa na maadui. Sasa tupo katika awamu ya mwisho ya operesheni na maeneo yote yaliyokaliwa na wananchi wasiokuwa na hatia ambao wanadhuriwa na al-Shabaab yatakombolewa."