Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amekemea tabia ya baadhi ya wazazi na
walezi kuwanyima fursa za kielimu watoto wa kike, hatua ambayo inadumaza
maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Amesema moja kati ya malengo
makuu ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ni kuondoa ubaguzi wa aina
zote, sambamba na kuwapatia elimu watoto wote bila ya kuwepo ubaguzi wa
kipato au jinsia.
Maalim Seif ameeleza hayo leo
baada ya kufungua jengo la madarasa manne la skuli ya Mbuyutende jimbo
la Matemwe, ikiwa ni katika shamrashamra za maadhimisho ya miaka 49 ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema elimu ndio msingi wa
maendeleo kwa watoto, hivyo wazazi wanapaswa kuwapatia elimu watoto wao,
ili kuhakikisha kuwa wanawajengea mazingira bora ya maisha yao ya
baadae.
Sambamba na hilo Maalim Seif
ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuangalia uwezekano wa
kuifanyia marekebisho mitaala yake ya elimu, ili iendane na wakati na
kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
“Wapo vijana wengi wamemaliza
hadi vyuo vikuu lakini hawana ajira, kwa hivyo mitaala yetu hii lazima
iwaandae vijana waweze kujiari wanapohitimu masomo yao”, alifahamisha
Maalim Seif.
Kuhusu upungufu wa walimu katika
skuli za vijijini Maalim Seif amesema tatizo hilo linachangiwa na
ukosefu wa nyumba za walimu, na kutoa wito kwa Wizara ya Elimu
kushirikiana na serikali ya Mkoa huo kutafuta nyumba za walimu ili
kuondosha tatizo hilo.
“Ukosefu wa nyumba za walimu ndio tatizo la msingi la upungufu wa
walimu katika skuli za vijijini, kwa hivyo Wizara ya Elimu shirikianeni
kwa karibu na Mkoa pamoja na Halmashauri kutafuta nyumba ijapo za
kukodi, ili walimu wanaotoka mbali wapate mahali pazuri pa kuishi”,
aliagiza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Amali Mhe. Ali Juma Shamuhuna ameahidi kukamilisha upatikanaji wa
madawati katika skuli hiyo, ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira
bora.
Katika risala ya wananchi wa
kijiji cha Mbuyutende iliyosomwa na nd. Makame Juma, wananchi hao
wamesema licha ya mafanikio waliyoyapata katika kijiji hicho, bado
wanakabiliwa na matatizo kadhaa yakiwemo ukosefu wa maji safi na salama,
umeme na barabara.
Katika hafla hiyo jumla ya shilingi milioni 11 na laki nne
zimechangwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo jipya la skuli hiyo
ambapo Maalim Seif ameahidi kuchangia shilingi milioni tano.