Thursday, December 13, 2012

CCM,CUF WAVUTANA MASHATI ZANZIBAR


Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) vimeshutumiana vikali kuhusiana na kuvunjika kwa mikutano miwili ya kutoa maoni ya katiba Visiwani Zanzibar juzi. CCM wamesema vurugu zinazotokea katika vituo vya kutoa maoni ya katiba zinaratibiwa na CUF na kutaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuchukua hatua dhidi ya watu walioamua kuvunja sheria. Tamko hilo lilitolewa jana na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Zanzibar, Issa Haji Gavu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar. “Haya yanayofanyika sasa na kutokea ni matendo maovu, ni uhalifu na zaidi yakitaka kuturudisha tena katika zama nyeusi za mivutano, malumbano na kujenga upya uhasama,” alisema Gavu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar. Alisema CUF imekuwa ikisafirisha wafuasi wake wanaotetea Muungano wa mkataba katika magari kwenda kutoa maoni katika maeneo wasiyoishi na kusababisha vurugu kati yao na wakazi halali katika maeneo hayo. Gavu alisema watu wanaosafirishwa siyo wenye ulemavu wa viungo, lakini wanalazimika kusafirishwa kwa magari kwa kuwa ni wageni katika maeneo wanayokwenda kutoa maoni. “Matukio haya kwa sehemu kubwa yana lengo la kuleta mmomonyoko wa kutovumiliana na kutostahamiliana kulikoanza kustawi na hivyo kujenga wasiwasi na hofu,” alisema Gavu. Hata hivyo, alisema kwamba pamoja na wanachama wa CCM kuzomewa wanapotoa maoni kuhusu kuendelea kwa mfumo wa Muungano wa serikali mbili, CCM itaendelea kutetea mfumo huo kwa nguvu zake zote kwa vile ndiyo msingi wa ilani yake ya uchanguzi ya mwaka 2010-2015. “Tunaamini kuwa maoni na mawazo ya kila mwananchi kwa ajili ya uundwaji wa katiba mpya ni sehemu ya utekelezaji wa misingi ya demokrasia na mtu yeyote hapaswi kuwekewa mipaka au ukomo wa kutoa mawazo yake,” alisema. Alisema kuwa CUF imekuwa ikipandikiza watoa maoni mamluki ambao tayari wametoa maoni katika majimbo yao baada ya kuona wananchi wanaotaka mfumo wa Muungano wa serikali mbili ni wengi katika shehia mbalimbali. “Ili uonekane bingwa, mwenye uchungu na Zanzibar, mzalendo wa kweli na mwana mageuzi makini, unalazimishwa utoe maoni yanayopendekeza mfumo mpya wa Muungano wa mkataba na hutakiwi utoe maoni ya serikali mbili, huu ni uvunjaji wa misingi ya demokrasia,” alisema Gavu. CUF YAJIBU Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari na Uenezi wa CUF, Salum Bimani, alikanusha chama hicho kuhusishwa na matukio ya vurugu hizo na kusisitiza kwamba zinafanywa na wabunge na wawakilishi wa CCM. Alisema viongozi hao wamekuwa wakikusanya watu katika matawi ya CCM na kuwapeleka kutoa maoni ya Katiba kwa kutumia utaratibu maalum wa kupangwa mwanzo na kuwanyima haki watu wanaoonekana kuwa ni wafuasi wa vyama vya upinzani. Aliwataka baadhi ya wabunge na wawakilishi wa CCM (majina tunayahifadhi) kuwa wamekuwa wakifanya kazi ya kupeleka watu kwenda kutoa maoni yanayoinga mkono ya Muungano wa serikali mbili. Bimani alidai kuwa pamoja na Tume hiyo kuongozwa na wanasiasa wakongwe na watu wanaoheshimika katika jamii wakiwamo Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba; Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhan na Waziri Mkuu Mstaafu, Salim Ahmed Salim, lakini kazi imewashinda kutokana na majukumu ya tume kutekwa na viongozi wa CCM Zanzibar. Alisema wananchi wamekuwa wakikusanywa na kupewa posho na kupikiwa pilau mambo ambayo yalitakiwa kukemewa na Tume na kuchukua hatua kali dhidi ya watu na viongozi wanaofanya vitendo hivyo. KAULI YA WARIOBA Kwa upande wake Warioba, alijibu madai ya Bimani na kusema kuwa vyama vya siasa vikae pembeni na kuwaacha wananchi watoe maoni yao bila kuingiliwa wala kushinikizwa. Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Jaji Warioba alisema wao wanafanya kazi ya kuchukua maoni ya wananchi na kwamba hawasikilizi vyama vya siasa vinasema nini. “Sisi bado tunaendelea na kuchukua maoni ya wananchi ili waweze kupata katiba mpya na wala hatusikilizi na kuangalia vurugu za vyama vya siasa,” alisema na kuongeza: “Tunavitaka vikae pembeni na kuwaacha wananchi.” Alisema mchakato wa kukusanya maoni unahusu wananchi na kwamba hawataki kufanyi kazi ya kulumbana na vyama vya siasa na kuacha kazi waliyopewa. POLISI WAZUNGUMZA Jeshi la Polisi Zanzibar limesema mabishano makali yaliyoibuka katika vituo vya kutoa maoni ya Katiba ndiyo chanzo cha mikutano miwili kuvunjika. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumzia vurugu za juzi zilizosababisha kuvunjika kwa mikutano miwili katika majimbo ya Mpendae na Magomeni. Alisema mabishano hayo yamekuwa yakitokana na kundi moja la wananchi kulalamika kuwapo watu wanaojitokeza kutoa maoni wakati siyo wakazi halali katika maeneo ambayo mikutano hiyo inafanyika. Hata hivyo, alisema jeshi hilo tayari limechukua hatua mbalimbali kuhakikisha tume hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake ikiwamo kuimarisha ulinzi. Kamanda huyo alisema kuwa hadi jana hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa.

MATOKEO YOTE YA MAONI JUU YA KATIBA MPYA KWA SIKU YA LEO


NA HAMED MAZROUY
KUFUATIA MWENDELEZO WA UTOWAJI WA MAONI JUU YA KATIBA MPYA ULIOENDELEA KATIKA SHEHIA YA JANGOMBE ASUBUHI YA LEO WANANCHI WALIOTAKA ZANZIBAR HURU IKIFUATIWA NA MUUNGANO WA MKATABA KATI YAKE NA TANGANYIKA NI 73.
NA KWAUPANDE WAO WANANCHI WALIOTOWA MAONI YAO NA KUTAKA MFUMO HUU WA MUUNGANO ULIOPO UENDELEE KUBAKI KAMA ULIVO LAKINI UFANYIWE BAADHI YA MAREKEBISHO NI 81.
TUME HIO ILIENDELEA TENA NA UKUSHANYAJI WAKE HUO KWA WAKATI WA JIONI HUKO KATIKA SHEHIA YA MIGOMBANI AMBAPO WANANCHI WALIOTOWA MAONI YAO KATIKA SHEHIA HIO NA KUTAKA ZANZIBAR HURU YENYE MAMLAKA KAMILI KITAIFA NA KIMATAIFA IKIFUATIWA NA MUUNGANO WA MKATABA KATI YAKE NA TANGANYIKA NI 92.
NA KWAUPANDE WAO WANANCHI WALIOTOWA MAONI YAO NA KUTAKA MUUNGANO HUU ULIOPO UENDELEE KUBAKI KAMA ULIVO HIVI SASA LAKINI KUREKEBISHWE KWA BAADHI YA KASORO NI 64

ANGALIA UUMBAJI WA ALLAH NA UWEZO WAKE

Photo: Extraordinary fashion shoot involves whale sharks, world's largest fish.

READ HERE: http://bit.ly/TersHd 

Photo: Popularity soars for rare bottlenose dolphin named 'Patches'.

READ HERE: http://bit.ly/RIrwh4 


Photo: Extraordinary white humpback whale documented off Norway. 

READ HERE: http://bit.ly/QMndUS 

 Photo: XCEL releases HECS wetsuit, a technology they say may reduce aggression from sea life.

READ HERE: http://bit.ly/Urf8pT 

Photo: Diver's capture of a beloved giant Pacific octopus sparks outrage

READ HERE: http://bit.ly/RSI2Je 

Photo: Photographer becomes focus of large and ferocious mako shark.

READ HERE: http://bit.ly/R7rgWj

Kamati ya Baraza la Wawakilishi yatembelea Redio jamii Micheweni - Pemba


 Wajumbe wa Kamati ya baraza la wawakilishi
Wajumbe wa Kamati ya baraza la wawakilishi
WAMWANZO kushoto ni Kaimu Meneja wa radio Jamii Micheweni (RJM) Pemba, Ali Massoud Kombo akitoa maelezo mbele ya Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari ya Baraza la Wawakilishi, kuhusu kazi na changamoto za radio hiyo kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Asha Bakar Makame, akifuatiwa na Naibu Waziri wa Habari Hindi Hamad Khamis wakati kamati hiyo ilipotembelea kituo hicho jana

Bodi ya Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar yazinduliwa


Waziri wa habari Mh,Said Ali Mbarouk akiwa pamoja na wajumbe wapya wa bodi ya chuo cha uandishi wa habari Zanzibar
Waziri wa habari Mh,Said Ali Mbarouk akiwa pamoja na wajumbe wapya wa bodi ya chuo cha uandishi wa habari Zanzibar
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk, amesema kuinua tathnia ya habari nchini kutapelekea kukuza uchumi wa taifa na hatimae kupatikana kwa maendeleo kwa haraka zaidi nchini.
Kauli hiyo ameitoa leo katika uzinduzi wa bodi mpya chuo cha uandishi wa habari na mawasiliano ya umma Zanzibar uliofanyika katika ukumbi wa chuo hicho Vuga Mjini Unguja.
Waziri Mbarouk amesema  hayo leo (Jumatano 12 Disemba) wakati akiizindua rasmi bodi mpya ya chuo hicho yenye lengo la kukuza na kuimarisha mazingira bora ya chuoni hapo ili chuo hicho kiweze kuzalisha wasomi bora katika tasnia ya habari na wenye kuchochea upeo wa maendeleo hasa katika upande wa Uchumi wa chi yetu.
Pia amesema, changamoto kubwa zinakikumba chuo hicho ni kutokua na madarasa ya kutosha pamoja na ofisi ya kutendea kazi,hivyo ameitaka bodi hiyo mpya kutilia mkazo masuala hayo ili kupatikane mazingira mazuri yenye kuleta matarajio mema katika maendeleo ya chuo hicho.
Nae kwa upande wake mwenyekiti mpya wa bodi hiyo, Chande Omar Omar asema,kupitia wajumbe wenzake watachukua jitihada mbadala za kuweza kuweka mazingira safi Pamoja na upatikanaji wa elimu iliobora chuoni hapo kwa kuzingatia sheria na kanuni za chuo hicho.
Aidha ameendelea kusema kuwa kwa kushirikiana na wizara ya habari bodi hio watatafuta wafadhili mbalimbali watakao weza kuleta maendeleo ya chuo hicho.
Sambamba na hayo ametoa shukradhi za dhati kwa waziri huyo kwakuweza kuungana pamoja kutekeleza kazi zao ambazo zinalenga kuweka mazingira bora ya chuo hicho.
Bodi iliopita imekwisha muda wake tarehe 9 june mwaka huu,na bodi mpya imezinduliwa leo tarehe 12/12/1012 ambayo inawajumbe kadhaa miongoni mwa wajumbe hao ni mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar,  Yussuf Omar Chunda, Bi Najma Khalfan na wengineo, pia hafla hio ilihudhuriwa na walimu na baadi ya wanafunzi wa chuo hicho.

Mchango wa mawasiliano kwenye MKUZA


KATIBU MTENDAJI WA TUME YA UTANGAZAJI ZANZIBAR ND, CHANDE OMAR CHANDE
Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Chande Omar
Iwapo itatumika ipasavy, sekta ya mawasiliano inaweza kuwa na mchango mkubwa sana katika kuufanikisha Mpango wa Kitaifa wa Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA).
Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Chande Omar wakati akifungua semina ya siku mbili juu ya mkakati wa mawasiliano katika MKUZA katika ukumbi wa hoteli ya Bwawani.
Chande amesema kuwa elimu inahitajika kutolewa kwa wananchi kujua dira na dhamira ya serikali katika mpango huo ili kuweza kufikia mafanikio.
“Jamii inahitaji kupewa taarifa mbali mbali kupitia vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii ili kupata taarifa muhimu.“ Amesema Chande.
Naye Kamishna wa Ukuzaji Uchumi kutoka Wizara ya Fedha na Uchumi, Dk. Rahma Mahfoudh ameutolea ufafanuzi kuhusu MKUZA II juu ya kutokomeza umasikini Zanzibar.
Akizungumza katika ufunguzi wa semina hiyo Kamishna wa Mawasiliano Ikulu, Hassan Khatib, amesema kuwa kukosekana kwa uwelewa wa MKUZA kwa wananchi ni jambo linalokwamisha juhudi za serikali kufikia malengo yake ya kuondosha umasikini.

Sekta ya uvuvi imeimarika – Wizara


zanzibar-fish-blue-marlin
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imeeleza kuwa sekta ya uvuvi hivi sasa imezidi kuimarika baada ya wananchi wengi kushajiika na kuanza kufuga mazao ya baharini kwenye maeneo yao wanayoishi. Aidha, Wizara hiyo ilieleza kuwa uzalishaji wa mwani umeongezeka kutoka tani 12,516 mwaka 2010 mpaka tani 13,040 mwaka 2011 ikiwa ni ongezeko la asilimia 4 na kuelezea mafanikio zaidi katika sekta ya uvuvi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa shughuli za ufugaji wa viumbe vya baharini kama vile samaki, kaa, kasa, majongoo na chaza.
Maelezo hayo yametolewa na uongozi wa Wizara hiyo, wakati wa mkutano kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika kuangalia utekelezaji wa Malengo Makuu ya Wizara hiyo kwa kipindi cha Aprili- Juni 2011-2012 na Julai- Septemba 2012-2013. Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee alishiriki kikamilifu, Wizara hiyo ilieleza kuwa mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.1 mwaka 2010 hadi 6.7 mwaka 2011.
Akisoma taarifa ya utangulizi ya utekelezaji wa Malengo makuu hayo ya Wizara, Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdilahi Jihad Hassan alisema kuwa kiwango cha uvuvi wa samaki kimeongezeka kutoka tani 25,693 mwaka 2010 na kufikia tani 28,759 mwaka 2011 ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.6. Pia, Waziri Jihadi alieleza mafanikio mengine katika Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuanzisha mabwa mawili ya mfano ya kufugia samaki katika maeneo ya kiungoni na Pujini Pemba kama ni mashamba darasa kwa wafugaji wa samaki.
Kuongezeka kwa idadi ya samaki kulikotokana na kuimarisha usimamizi kwa maeneo ya hifadhi na kuendelea kutoa elimu kwa wavuvi pamoja na kuongezeka kwa taaluma juu ya athari ya matumizi ya mitego haramu na njia haramu za uvuvi. Pamoja na hayo, Wizara hiyo ilieleza mafanikiokatika sekta ya mifugo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mwamko wa ufugaji wa ngombe na mbuzi wa maziwa na kuku wa kienyeji ambapo jumla ya shamba darasa 180 za mbuzi wa maziwa, ngombe wa maziwa na kuku zimefanywa.
Uongozi huo pia, ulieleza kuwa Wizara imeandaa mipango kwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 ambapo miongoni mwa vipaumbele ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari, kutoa nafasi za ajira kwa vijana kupitia shughuli za ufugaji na uvuvi na kufanya utafiti juu ya maradhi ya mifugo. Akitaja miongoni mwa changamoto zilizomo katika sekta ya mifugo na uvuvi, Waziri Jihadi alisema kuwa nia pamoja na uhaba wa wataalamu wa fani ya ufugaji wa mazao ya bahari ambapo hivi sasa Wizara imo katika juhudi za kuwasomesha wafanyakazi katika Chuo cha Mbegani na tayari baadhi yao wamepekwa nchini India, China na Korea.
Uharibifu wa makaazi ya samaki unaosababishwa na matumizi ya uvuvi haramu wa nyavu za macho madogo, nyavu za kukokota na mfumo mbaya wa mitego inayobuniwa na wavuvi, ambapo tayari Wizara imeanzisha doria pamoja na kutoa elimu kwa wavuvi. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein pia, alikutana na uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na kuelezea utekelezaji wa Malengo Makuu ya Wizara hiyo kwa kipindi cha Aprili- Juni 2011-2012 na Julai- Septemba 2012-2013.
Ukitoa maelezo yake hayo, uongozi wa Wizara hiyo chini ya Waziri wake Mhe. Rashid Seif Suleiman, ulieleza kuwa imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kusimamia maendeleo ya sekta ya usafiri na mawasiliano kwa kufuata muongozo wa bajeti ya Serikali unaosisitiza utekeleza wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA II), pamoja na maelekezo ya Rais. Waziri Suleiman alieleza kuwa Wizara yake imeweka vipaumbele katika kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na bandari pamoja na uimarishaji wa huduma za mawasiliano.
Alisisitiza kuwa utekelezaji wa vipaumbele hivyo unaendana na utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA II 2010-2015) ambayo pia, yamezingatia Dira ya maendeleo ya Karne ya 2020. Pamoja na hayo, Wizara hiyo ilieleza kuwa kazi ya uwekaji wa kifusi kwa tabaka la mwisho pamoja na matayarisho ya uwekaji wa lami ya maji zimefanyika katika barabara za Wete-Konde yenye kimolita 15.1 na barabara ya Wete-Gando yenye urefu wa kilomita 13.6.
Aidha, Wizara hiyo ilieleza kuwa kazi za matayarisho ya ujenzi ikiwemo upimaji wa eneo la ujenzi wa barabara za Koani-Jumbi yenye urefu wa kilomita 6.3 na Jendele- Cheju-Kaebona yenye urefu wa kilomita 11.7 zimefanyika. Akitoa maelezo yake kwa njakati tofauti alipokutana na viongozi na watendaji wa Wizara hizo, Dk. Shein alitoa pongezi zake kwa juhudi kubwa zilizochukuliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kusisitiza kuwa mafanikio waliyoyapata yametokana na mashirikiano makubwa waliyonayo.
Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein aliutaka uongozi huo kuongeza ushirikiano wao ili waweze kupata mafanikio makubwa zaidi katika utendaji wa kazi zao na hatimae kuendelea kuletea maendeleo nchini huku akipongeza jinsi Wizara hiyo ilivyowasilisha Bangokitita lake kwa ustadi mzuri. Pamoja na hayo, Dk. Shein alipokutana na uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano alipongeza juhudi inazozichukua Wizara hiyo katika kutekeleza kazi zake kwa upande wa Unguja na Pemba.
Stori na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

CHAMA cha soka Zanzibar ZFA kimeombwa kuwashirikisha na kuwa nao karibu wachezaji waliowahi kuwika zamani, ili kuchota taaluma ya kukuza soka hapa nchini.

Kisiwa cha Pemba
Kisiwa cha Pemba

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti wanandika hao wa zamani waliovuma na timu za Tamasha na Mkoani Shooting za Mkoani, walisema wanashangaa kuona ZFA haiwatumii katika masuala ya soka. Walisema kuwa wao wanayo mengi ya kukipa chama hicho, lakini wamekuwa hawashirikishwi katika mipango na mikakati yao, jambo ambalo linawashangaaza sana.
Salim Abdallah Kiburungu, alisema haoni kwamba ZFA inayoa azama na nia ya kweli ya kukuza kiwango cha soka hapa nchini, kutokana na kutokuwa na mipango ya kweli juu ya hilo.
Kiburungu ambaeo aliwahi kukipiga na timu ya taifa ya Zanzibar na Tanzania, alifafanua kuwa, ikiwa kweli ZFA inataka kuendeleza mbele soka na Zanzibar kutisha kama enzi zao, ni vyema kuzilazimisha timuz zote wanazoziongoza kuhakikisha wanakua na timu ndogo ndogo (vitalu)
‘’Sisi japo hazikuwa rasmi, lakini wakati wazee wetu wanacheza basi zilikuwepo timu ndogo ndigo na iwapo zile kubwa zinataka wachezaji basi kwanza wanaangalia zile zilizozpo na sio kuwenda kijiji chengine’’,alisema.
Ali Khamis Mtumweni ambae anae aliekuwa kuwa mchezaji wa timu ya faifa ya Zanzibar na Taifa Stars, alieleza kuwa pamoja na kwamba sasa ZFA inapata ufadhili kila wakati, lakini hado timu za Zanzibar zinapotoka nje ya Tanzania hazifanyi vyema.
Hivyo amekipa rai Chama hicho kuhakikisha kuwa, wanazinyanyua timu zilizoko madaraja madgo, kwani huko ndio vipaji vinakoanzia na sio kushughulikia timu kubwa ambazo zimechoka.
‘’ZFA kwa karne hii kama inadhamira ya kweli inaweza kukuza soka la Zanzibar, maana miundombinu inaruhusu sana lakini wengi wapo madarakani kwa maslahi yao binafsi na sio ya taifa hili’’,alifafanua Mtumweni.
Katika hatua nyengine Mshambuliaji huyo aliekuwa akikipiga na timu ya Tamasha ya Mkoani, aliwataka wachezaji kuwa na moyo wa kujitolea, uzalendo, uwajibikaji ili kuliletea heshima taifa hili.
Nae Foum Haji mchezaji wa zamani wa klabu hiyo ya Tamasha, alisema uwepo wa vilabu vyingi havinyanyui soka badala yake vimekuwa vikishushua soka kwani ushindani unaojitokeza hausaidii kwa taifa.
Hata hivyo alisema kwa sasa kama kweli vijana wanayonia ya kukuza soka na Zanzibar kuwa moto wa kuotea mbali, wanayonafanasi hiyo kutokana na miundombinua kuwa bora ikiwa ni pamoja na waalimu, wafadhili na maisha kuwa afadhali.
Hata hivyo amewataka wachezaji wa makocha wa kileo wasiache kuwatumia wao ili kuwapa mbinu na miongozo sahihi ya kufikia mafaniki yao katika soka

Mimi ni muumini wa mfumo wa muungano uliopo’- Waziri Mwinyihaji Makame


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapiznduzi, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapiznduzi, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapiznduzi, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini, amesema kuwa, yeye ni muumini wa mfumo wa Muungano uliopo na sio Muungano wa mkataba kama baadhi ya wananchi wanavyotaka.
Alisema kuwa, katika hilo yeye hamumunyi mdomo, wala hapati kigugumizi na anaamini mfumo uliopo hivi sasa wa serikali mbili, ndio unaofaa kwa pande mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.
Dk Mwinyihaji Makame Mwadini, alitumia fursa hiyo, kueleza hayo, huko katika ukumbi wa Misali Sunset Beach, Wesha Chake Chake Pemba, katika mkutano wa kikao cha tano cha ushirikiano, baina ya Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serekali za mitaa Zanzibar na wizara ya nchi ofisi ya waziri Mkuu tawala za mikoa na serikali za mitaa Tanzania bara.
Alikiri kuwepo kwa kero za Muungano ambapo, amesema kuwa zinafanyiwa ufumbuzi, na serikali zote mbili, na wala sio kuwepo kwa serekali ya mkataba kama wananchi wanavyodai.
“Mimi ni muumini wa Muungano wala hakuna Muungano wa mkataba kama baadhi ya wananchi wanavyodai katika sehemu mbali mbali”alisema Dk Mwinyihaji.
Alifahamisha kuwa, katika kushinda goli, lazima wananchi wadumishe Muungano, kudumisha udugu na kupiga vita adui ujinga na ukoloni mamboleo, sambamba na kuwataka wajumbe hao kusaidiana katika kujenga Zanzibar yenye amani na utulivu.
Aliongeza kuwa, katika kujenga nchi pamoja na kuendeleza elimu, mambo ya afya na huduma zote za kijamii kwa ustawi wa wananchi wao kama ilivyo lengo la vikao hivyo, ambavyo hujadili mada mbali mbali ambazo zitatoa mambo muhimu ambayo yatakayo wasaidia wananchi wotepamoja na kujua changamoto zinazowakabili katika ufanikishaji wa shuhuli zao.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serekali za mitaa Tanzania Bara ( ELIMU), Kassim Majaaliwa, alizitaka ofisi zote za bara na visiwani kulenga kutoa huduma bora kwa wananchi, hususana katika suala zima la elimu kwa watoto.
Alisema kuwa umefika wakati kwa wajumbe kuwa makini kuhakikisha wanatoa majibu mazuri, kama ililivyo lengo la serekali zote mbaili kuwahudumia wananchi wake kikamilifu na kuwatatulia kero zao.
“Niwajibu wetu kuyatekeleza hayo kwa wananchi, kwani wananchi wanatarajia kuona matunda mazuri kutoka katika kikao chetu hichi maalumu ambacho serikali nzima leo ipo hapa”alisema Naibu waziri Majaliwa.
Alifahamisha kuwa, kutokana na kuongezeka idadi ya watu, Rais Kikwete aliona ipo haja kwa kila kijiji kuweka shule ya msingi li kweza kuwapatia elimu watoto na kuwajengea mfumo mzima wamustakbali wa maisha yao ya baadae.
Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Aggrey Mwanri, amesema kuwa, ziara hizozitawasaidia katika kudumisha Muungano, kwa kujenga umoja, amani na upendo kwa viongozi wa serikali na wananchi kwa ujumla.
Aliwataka wajumbe wa mkutano huo, kujenga umoja na mshikamano ambao utakaoweza kuwapatia malengo ambayo yatakayo weza kuwaletea ushindi katika kazi zao za baadae za kuwahudumia wananchi