Friday, July 12, 2013

Wafuasi wa Morsi waandamana Cairo


Wafuasi wa rais wa zamani wa Misri Mohamed Morsi
Wafuasi wa rais wa Misri aliyeondolewa madarakani Mohammed Morsi wamefanya maandamano makubwa mjini Cairo, huku waumini wa dini ya Kiislamu wakiadhimsiha Ijumaa ya kwanza tangu kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadan.
Wafuasi wa kiongozi huyo wa vugu vugu la Muslim Brotherhood walijikusanya Mashariki mwa mji huo, kushinikiza utawala wa kijeshi kumrejesha madarakani kiongozi wao.
Wapinzani wa rais huyo wa zamani ambao waliandamana hadi rais huyo akaondolewa madarakani na jeshi watakusanyika katika medani ya Tahrir.
Watu kadhaa wameuawa kwenye ghasia zilizotokea tangu Morsi alipoondolewa.
Mwandishi wa BBC mjini Cairo, Jim Muir anasema vuguvugu la Muslim Brotherhood huenda liliwatenga raia wengi wakati wa utawala wa Morsi, lakini bado raia wengi wa nchi hiyo hawataki jeshi kuingilia masuala ya siasa.

Marekani kutuma ndege za kivita Misri

Siku ya Alhamisi serikali ya Marekani, ilitoa wito kwa utawala mpya wa Misri, kusitisha harakati zake za kuwakamata wanachama wa vuguvugu la Muslim Brotherhood na kuonya dhidi ya kulenga kundi lolote.
Wanajeshi wakishika doria mjini Cairo
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon vile vile ameonya utawala huo wa Misri kutotenga chama chochote cha kisiasa katika harakati za kutatua mzozo wa kisiasa unaokumba taifa hilo.
Hata hivyo msemaji wa Ikulu ya White House, Jay Carney amesema, utawala wa Washington hauamini kuwa ni lazima isitishe misaada yake ya Misri.
Marekani inatarajiwa kupeleka ndege nne za kivita aina ya F-16 nchini Misri, lakini haijathibitisha kuwa msaada huo utatolewa lini.
Serikali ya Marekani imesema, inachunguza ikiwa aumuzi huo wa jeshi la Misri kumuondoa madarakani rais Morsi ni mapinduzi ya Kijeshi kwa kuwa sheria za Marekani inazuia serikali kutoa misaada kwa nchi yoyote ambayo kiongozi aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia ataondolewa kupitia mapinduzi.
Wafuasi wa rais Morsi wamekuwa wakiandamana wiki nzima karibu na kambi ya kijeshi iliyoko Mashariki mwa mji mkuu wa Cairo, ambako wanaamini kuwa kiongozi wao anazuiliwa na maafisa wa kijeshi tangu alipoondolewa madarakani.

KAHABA AWATESA POLISI DAR




Mrembo mwenye ulemavu wa ngozi, Emmily Omari, 23, mkazi Buguruni, Dar anayedaiwa kujihusisha na biashara haramu ya uchangudoa, hivi karibuni alipandishwa kizimbani kwa madai ya kufanya kosa hilo.

Emmily ambaye amekuwa akiwatesa askari polisi ambao wamekuwa wakimkamata mara kwa mara na kumfikisha mahakamani lakini haachi tabia hiyo, alipandishwa katika Mahakama ya Jiji na kusomewa mashtaka yake.

Hakimu aliyekuwa akiendesha kesi hiyo, Timothy Lyon alipigwa butwaa kumuona mrembo huyo ambaye aliwahi kumhukumu zaidi ya mara tano kwa kosa la kujiuza na kumuachia huru baada ya kulipa faini.

Pilato huyo baada ya kumuona tena Emmily mbele yake akikabiliwa na shitaka lilelile, alimuuliza alikuwa na tatizo gani lililosababisha mara kwa mara afikishwe mahakamani hapo, mrembo huyo hakujibu chochote.

We Emmily sasa unatuletea utani, kila siku unaletwa hapa tunakupiga faini unalipa unatoka na kwenda kurudia hiyo biashara yako… sasa tunaona kama unatufanyia masihara sasa leo hakuna cha faini wala dhamana uende Segerea ukale dona la bure labda utajifunza,”
alisema Hakimu Lyon na kuwaamuru askari wampandishe kwenye Karandinga kwa ajili ya safari ya gerezani.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana juzikati zinaeleza kuwa mrembo huyo baada ya kukaa Segerea kwa wiki mbili, alipewa dhamana wakati mahakama ikiendelea kumjadili.

Uwanja wa Heathrow wafungwa kwa muda


Ndege ya aina ya Boeing 787 inayomilikiwa na Shirika la ndege la Ethiopia katika uwanja wa Heathrow
Shughuli katika uwanja wa ndege wa Heathrow zimekwama kwa muda baada ya ndege moja ya shirika la ndege la Ethiopia aina ya Boeing 787 Dreamliner kushika moto.
Safari zote za ndege katika uwanja huo zilisitishwa kuanzia saa kumi na nusu.
Kwa mujibu wa msemaji wa mamlaka ya uwanja wa ndege wa Heathrow, hakuna abiria aliyekuwa ndani ya ndege hiyo wakati wa tukio hilo.
Mapema mwaka huu ndege hamsini aina ya Dreamliners, zilisimamishwa kufanya kazi kutokana na matatizo ya mtambo wa Battery.
Mwezi April, ndege moja ya shirika la ndege la Ethiopia, ambalo limesemekana kuwa ndilo lililopata matatizo katika uwanja wa Heathrow, ilisafiri kutoka Adis Ababa hadi Nairobi kwa mara ya kwanza tangu mwezi Januari.
Picha zilizochapishwa kwenye mtandao wa Kijamii wa Twitter, zimeonyesha ndege moja katika uwanja huo ikiwa imezingirwa na magari ya kuzima moto.
Wafanyakazi wa idara ya kuzima moto ya baraza la mji wa London wamesema kuwa walikuwa tayari kushirikiana na maafisa wa kitengo cha kupambana na mikasa ya moto katika uwanja huo.