Thursday, November 29, 2012

HABARI ZA KIMATAIFA.


Umoja wa Mataifa waiunga mkono Palestina


Mahmoud Abbas
Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa imepiga kura kuitambua Palestina kama mwanachama mwenye hadhi ya mwanachama asiye kuwa dola, huku Israel, Marekani na Canada zikiwa miongoni mwa mataifa yaliyopinga hatua hiyo. Baada ya hotuba kutolewa na kiongozi wa Palestina, Mahmoud Abbas, na Balozi wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa, wajumbe 138 waliikubalia Palestina, 9 waliikatalia na 41 walijizuia kupiga kura zao, bila ya shaka zikiwemo Uingereza, Ujerumani na mataifa mengine kadhaa – mengi yao ya Ulaya.
Katika wakati ambapo mjadala kuhusu Muungano wa Tanzania umepamba moto visiwani Zanzibar, wachangiaji wengi kwenye mitandao ya kijamii waliokuwa wakifuatilia moja kwa moja Mkutano wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, wamesema kwamba “sasa ni zamu ya Zanzibar”, wakimaanisha kwamba ni wakati wa Zanzibar kujitoa kwenye Muungano na kuchukua kiti chake Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, kura ya leo haimaanishi kwamba tayari Palestina imetambuliwa kuwa taifa na dola huru, ingawa ni muhimu sana kwa heshima yao na aibu kubwa kwa Israel na Marekani.
Balozi wa Marekani, Susane Rice, amelaumu hatua ya Hadhara Kuu kuipa hadhi ya uwanachama usio wa dola Palestina akisema kwamba haitabadilisha chochote kwenye  maisha ya Wapalestina. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alisema kwamba msimamo wake unabakia ule ule wa dola mbili huru, ya Israel na Palestina, lakini lazima mataifa hayo yaishi kwa amani.