Saturday, December 1, 2012

USHAIRI

Kulikumba Jini

Kulikumba Jini
Utumwa naliopewa, nende kwa jini nifike
Hamshike sawasawa, nimfunge afungike
Ashindwe jipapatuwa, chupani nimfundike
Kisha nende panganikwe, silisili kumtia
Na vifaa nikapewa, na nyenzo za uhakika
Makombe hazinguliwa, ya kunywa na ya kupaka
Na kafara hasomewa, na hirizi hajivika
Alipo nikamfika, lengo kwenda mchukuwa
Halikuta kubwa jini, lisilo mfano wake
Tangu juu hadi chini, sioni khatima yake
Katikati msituni, ‘meketi kitini pake
Bali nisitetemeke, nili nikijiamini Read the rest of this entry

Ningekuwa Sikupendi

Ningekuwa Sikupendi
Ningekuwa Sikutaki
Ningekuwa sikutaki, sege nawe ‘singekaa
Nisingefanya dhihaki, usoni ningekwambia
‘Singejipatisha dhiki, wala ‘singeng’ang’ania
Lakini n’nabakia, sababu nakuashiki
‘Ngekuwa sikuhitaji, kale ningeshakwachia
‘Singekufaya mkwiji, nendapo nakuchukua
Hawa hayapiti maji, bilawe kukuwazia
Sababu ya yote haya, wewe kwangu kama taji
Ningekuwa sikupendi, siri ‘singekufanyia
‘Singeupiga umundi, na boso na tarazia
Kusema halinishindi, wazi nikakuwekea
Lakini nawe wajua, mapenzi hayana fundi
Read the rest of this entry

U Wapi Ewe Furaha?

U Wapi Ewe Furaha?
Ninakujua Furaha hu mja wa kusalia
Hu mja unayekaa daima ukabakia
Huja mara ukangia na mara ukapotea
Lakini hebu rejea! Read the rest of this entry

JENGO LA BEIT- EL- AJAIB LAPOROMOKA ZANZIBAR


Beit el Ajab yaporomoka

Jengo la Beit-el-Ajaib likiwa limeanza kuporomoka upande mmoja.

Jengo la Beit-el-Ajaib likiwa limeanza kuporomoka upande mmoja.
Jengo maarufu la kihistoria Zanzibar, Beit-el-Ajab (Nyumba ya Ajabu) limeporomoka usiku wa tarehe 1 Disemba 2012. Akizungumzia tukio hilo, mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe ambako ndiko liliko jengo hilo, Ismail Jussa, alikuwa na haya ya kusema kupitia mtandao wa Facebook: “Aibu iliyoje leo kufikia Beit-el-Ajaib kuanguka baada ya Serikali kupuuza hatua zote za kuwazindua kuwa jengo hilo liko katika hali mbaya. Katika kikao cha Bajeti cha Baraza la Wawakilishi cha mwezi Juni/Julai 2011 na 2012 nilizungumzia suala la uwezekano wa majengo haya ya kihistoria kuanguka kutokana na kutotunzwa au kufanyiwa matengenezo.
“Nikaandika na swali maalum kuhoji matengenezo ya majengo hayo hasa baada ya mradi wa MACEMP unaofadhiliwa na nchi wahisani na mashirika ya kimataifa kuwa na fungu la matengenezo la majengo ya Kasri (Palace) na Beit-el-Ajaib. Kama kawaida ya majibu ya Serikali, tuliambiwa, ‘Tusiwe na wasiwasi’. Nikatahadharisha kuwa binafsi nimeyatembelea majengo hayo mawili kuona pamefanyika matengenezo gani kutokana na fedha zilizotengwa, na kuona hapana matengenezo ya maana. Nikajibiwa, ‘Tutafuatilia’. Sasa leo hii turathi ya kitaifa (national heritage) ambayo ni jengo la kwanza refu katika Afrika Mashariki, la kwanza kuwa na umeme na la kwanza kuwa na lifti kiasi cha kuitwa Jumba la Ajabu (House of Wonders) limeanguka kwa uzembe wa Serikali. Shame on them!”
Naye mwandishi wa habari wa siku nyingi visiwani Zanzibar, Ally Saleh alikuwa na haya ya kuandika kulilia jengo hilo ambalo limekuwa alama ya Zanzibar kwa karne na karne:

POLISI AJERUHIWA ZNZ

Polisi ajeruhiwa kwa mapanga Zanzibar

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa
Watu wasiojulikana wamemvamia askari polisi mmoja na kumjeruhi kwa mapanga, mnamo majira ya saa 10:00 alasiri katika huko Mboriborini kando kidogo ya mji wa Zanzibar. Imeripotiwa kwamba kundi hilo la watu lilimvamia askari huyo anayejulikana kwa jina la Othman Juma na kufanikiwa pia kuchukua pesa alizokuwa nazo ingawa haijajulikana ni kiasi gani mpaka sasa. Hatua za kumpatia matibabu askari huyo zinaendelea vizuri katika hospitali ya Al Rahma, Kilimani Unguja.

KINUNI


Kinuni wataka Zanzibar huru ikifuatiwa na Mkataba

kinuni
Wananchi Kinuni wataka Zanzibar yenye mamlaka kamili ikifuatiwa na Muungano wa Mkataba.
Katika kukusanya ya Maoni ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano, watu wa shehia ya Kinuni, wilaya ya Magharibi Unguja, wamesema wanataka kuiona Zanzibar ikiwa huru kwanza, halafu pawe na Muungano wa Mkataba kati yake na Tanganyika. Jumla ya watu 135 walitoa msimamo huo mbele ya wajumbe wa Tume ya Katiba  juu ya katiba, huku  44 wakitaka mfumo wa sasa wa Muungano ubakie kama ulivyo.

NSSF YATOA MAELEZO DHIDI YA MALENGO YAKE


NSSF yatoa maelezo dhidi ya malengo yake

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Tanzania Dk.Ramadhani .K.Dau

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Tanzania Dk.Ramadhani .K.Dau
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Tanzania Dk.Ramadhani .K.Dau, akitowa maelezo ya Malengo ya baadae ya NSSF,kwa Wanachama wake na Jamii kwa ujumla wakati wa semina na Jukwaa la Wahariri Tanzania, uliofanyika katika hoteli ya Sea Cliff Mwangapwani Zanzibar.

KIMR. KWETE, NA MR. SHEIN MWAUMBUKA ZANZIBAR- KWANZA



Kikwete, Shein mwaumbuka Zanzibar – Sehemu ya Kwanza

Uchambuzi huu wa Ahmed Omar unaangazia hatima ya Maridhiano ya Wazanzibari mikononi mwa Chama cha Mapinduzi ambapo unahojia kwamba ndani ya kundi la wahafidhina wa CCM Zanzibar wakishirikiana na kundi la watawala Dodoma, kuna dhamira ya kuyafelisha Maridhiano hayo na kuuvunja Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Zanzibar Daima inauchapisha uchambuzi kama sehemu ya jukwaa la maoni. Endelea kusoma….

Je, uongozi wa juu wa CCM hauna imani ya kweli na Maridhiano ya Wazanzibari.

Je, uongozi wa juu wa CCM hauna imani ya kweli na Maridhiano ya Wazanzibari.
Maridhiano ya Wazanzibari hayakutoka Dodoma na kuna kila ushahidi kuwa hayakupata Baraka za Dodoma. Maridhiano ya Wazanzibari hayakutoka kwa wahafidhina, maagenti wa Dodoma walioko Zanzibar na halkadhalika kuna kila aina ya ushahidi sio tu hayakupata baraka zao lakini waliyapinga na wanaendelea kuyapinga kwa nguvu zao zote. Shabaha ya kupinga maridhiano ya Wazanzibari na serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kujenga farka, fitna, chuki, ukabila, ugozi, chokochoko na uvunjifu wa umoja na mshikamano miongoni mwa wazanzibari ili kurejesha hali kama ilivyokuwa huko nyuma. Lengo ni kwamba Dodoma (mkoloni mpya wa Zanzibar) aendelee kuitawala Zanzibar na mawakala wao (wahafidhina wa Zanzibar) waendelee kujaza matumbo yao huku wazanzibari walio wengi wakiteseka ndani ya ardhi yao tukufu.

Lengo kuu la mtandao huu wa kupinga maridhiano ni kujaribu mbinu hii na ile ili kuizima nuru njema ya umoja wa wazanzibari ambayo ndio silaha pekee wanayoitegemea hivi sasa katika kuirejesha Jamhuri ya watu wa Zanzibar. Lengo ni lile lile linaliandaliwa na “system” chini ya watawala wa Jamhuri ya Muungano na vibaraka wao wa Zazibar kuwa wazanzibari wasambaratike, wagombane, wasiwe wamoja, wasiaminiane na wasisikilizane.
Wanamtandao wanafahamu kwamba Wazanzibari wakiwa wamoja wanapata jukwaa la pamoja la kujadili na kusahau mawazo ya tofauti zao za kisiasa na huhisi machungu ya kudhalilika kwa nchi yao. Ukiwaondoa wazanzibari katika maelewano na umoja kwa kujenga mazingira ya kila upande uone bado sisi ni maadui kumbe baina yetu unafanikisha mpango wa kuwagawa katika agenda tunayoipigania.Mbinu kubwa wanayotumia maadui hawa wa Zanzibar hivi sasa ni ile ya kuandaa matukio mbali mbali na kuyanasibisha matukio hayo na UAMSHO kwa upande mmoja na kwa upande wa pili wakifanya kila wawezalo kuziunganisha harakati za UASHO na zile za chama cha CUF na kuziundia harakati zote mbili picha ya uongo zionekane kuwa zipo chini ya mwamvuli mooja na amri moja.
Lakini hebu tujiulize hivi hapa maadui hawa wa Zanzibar wamekuja na staili mpya? Haya ni mambo makongwe kabisa kwa Zanzibar ambayo yameshazoeleka. Kwa lugha nyengine hizi ni propaganda za kitoto kwa wazanzibari, hakuna jipya.Siku ya tarehe 3 Machi 1996, enzi zile wazanzibari walipogawanywa na kutiwa chuki baina yao ilidaiwa na serikali kuwa mafiasa watatu wa usalama waliokuwa kwenye doria huko katika kijiji cha Shengejuu, kisiwani Pemba, walipigwa na kuporwa silaha na wanakijiji. Kwa sura ya kawaida ya uaskari ni vigumu kuaminika kwamba askari watatu wakiwa na silaha mikononi waporwe silaha zao wote watatu na wapigwe bila ya wao hata kujeruhi mtu yeyote au kujeruhiwa wao wenyewe.
Muda sio mrefu, siku ya pili yake tu, kijiji hicho kilivamiwa na kiasi cha askari wapatao 300 wa kikosi cha FFU na jeshi la wananchi (JWTZ) waliokuwa wako kamili kivita. Unyama, mateso na vitendo vya kihuni walifanyiwa wananchi wa kijiji cha Shengejuu. Sio tu unyama huo walifanyiwa washukiwa, lakini pia mateso yaliwakuta watu wengi waliokuwa hawana hatia yoyote. Baadhi ya wanakijiji walipigwa hadi kuzirai, wengine waliibiwa mali zao kama vile kuku na mbuzi, maduka yaliporwa, wanawake walibakwa na watu wapatao 80 waliwekwa ndani.
Kati ya watu hao 80, watu 30 waliachiliwa huru na waliobaki waliendelea kusota ndani kwa kipindi kirefu sana. Kiongozi mmoja mkuu wa SMZ wakati ule, aliwahi kufanya mkutano na waandishi wa habari kuelezea hali ya mtafaruku inayoendelea katika kijiji hicho cha Shengejuu, na hapa namnukuu moja ya kauli zake aliyoitoa kupitia kikao hicho“Sasa tunataka kuwafanya watu wajue kama serikali ipo”.
Katika enzi hizo wafuasi wa CUF walikuwa wakisingiziwa kuhusika na hujuma mbalimbali kama vile kuchomwa moto madarasa ya skuli, kupaka vinyesi kwenye kuta za skuli, kutia vinyesi kwenye visima n.k. Hizi bila shaka zilikuwa ni mwendelezo wa propaganda chafu za kisiasa zilizokuwa na lengo la kujenga picha ya uongo na kuhalalisha hujuma dhidi ya watu wasio na hatia. Waliokuwa wakifanya haya ni watu waliofundishwa vyema propaganda na siasa chafu za uchochezi. Wakitekeleza vitendo hivyo huku wakilindwa na askari polisi.
Madhumuni ni kuendelea kupata fursa ya kuwatesa raia wasio na hatia kwa kuwapiga, kuwaweka gerezani na kuwaua. Waliokuwa wakifanya vitendo hivyo hawakujua kwamba walikuwa wanaonekana na wanafuatiliwa nyendo zao na hivyo kufahamika wao na waliowatuma.
Mkasa wa Shengejuu 1996
Katika hatua nyengine Siku moja wanakijiji hao hao wa Shengejuu katika nyakati za usiku wakiwa katika doria yao ya kuangalia ni nani hasa wanaofanya vitendo hivi, walifanikiwa kuwafumania watu hao. Wakiwa wanaendelea na doria, wanakijiji hao waliiona gari yenye namba za usajili ZNZ-12633 inayomilikiwa na usalama wa taifa ikisimama kiasi cha umbali wa mita 100 hivi kutoka ilpokuwepo skuli ya Shengejuu (Soma kitabu cha Dr. Mohamed Bakari, 2001 kiitwacho The Democratization Process in Zanzibar).
Ghafla watu watatu waliokuwa na galoni la mafuta ya petroli walishuka kutoka katika gari hiyo. Haraka haraka wakamwaga mafuta na kuchoma baadhi ya majengo ya shule hiyo na kukimbia. Wanakijiji wakajitokeza ghafla na kuwazingira wahalifu hao. Lakini mara milio ya risasi hewani ikasikika na watu hao kuingia ndani ya gari yao na kukimbia. Wanakijiji waliwahi kuuzima moto huo. Ilithibitika kuwa watu waliofanya vitendo hivyo ni wanamaskani waliokuwa wakilindwa na wanausalama ndio waliokuwa wakitekeleza vitendo na hujuma zile kwa nia ya kukizulia chama cha CUF na kuwatesa raia bila ya hatia yoyote kwa maslahi binafsi ya kisiasa.
Wimbi la Mageuzi Zanzibar lawatisha wahafidhina na watawalaMaadui wa Zanzibar baada kuliona wimbi la kudai mabadiliko katika mfumo na muundo wa Muungano wa Tanzania linaongezeka wameamua kujipanga upya na kujaribu kuwasambaratisha wazanzibari ili wasifikie lengo lao kwa kupitia mbinu hizo zilizotumika huko nyuma za kuandaa uongo na kuupandikiza katika jamii. Bila shaka wakitarajia uongo huo utaweza kuzaa chuki na fitna miongoni mwa makundi mabali mbali yaliyoshika kamba ya pamoja kutafuta maslahi ya nchi yao na hivyo kuiwachia kamba hiyo na kusambaratika.
Chuki ambazo zinajengwa hapa ni baina ya CUF na CCM kwa vitendo kama vile vya kuzichoma moto maskani za CCM na kuwasingizia CUF. Kuwatesa wafuasi wa CUF kwa visingizio mbali mbali kama vile kupambana na UAMSHO ili wafuasi wa CUF wakasirike na serikali na chao kwa kuwa CUF ni sehemu ya serikali hiyo. Wafuasi wa CUF wakikasirika dhidi ya chama chao itakuwa tayari umefanikisha kulisambaratisha kundi kubwa linashikilia engine ya kudai mabadiliko na hivyo kuliwacha kundi hilo likiwa dhaifu.Maadui hawa wa Zanzibar wameunda makundi maalum ya uharamia kama vile Ubaya Ubaya, Mbwa Mwitu na mengineyo. Makundi yote hayo yakitoka katika kundi kuu la awali la MAJANJAWIRI. Inaeleweka kwamba janjawiri ni vijana waliochukuiwa kutoka katika maskani za CCM na kupewa mafunzo ya kiaskari kwa lengo la kuajiriwa katika vikosi vya SMZ.
Baada ya kukosa ajira vijana hawa hupewa ajira ya muda ya kufanya hujuma mbali mbali ili kutimiza maslahi binafsi ya chama cha CCM. Hivi sasa majanjawiri wakiwa katika vikosi vipya vya ubaya ubaya na mbwa mwitu wamekuwa wakiratibu na kutekeleza vurugu barabarani, kuchoma moto matairi, na kuchoma moto maskani na makanisa. Halkadhalika vijana hawa ambao ni wepesi wa kuuwa ndio wanaotumika kufanya mauwaji na kisingiziwa vijana wa UAMSHO.Mkasa wa Baa ya Mbawala 2012
Kuna taarifa za uhakika za kikao cha CCM mkoa wa Mjini magharibi kilichosimamiwa na mwenyekiti wake Borafia Silima cha kupanga hujuma za uchomwaji moto wa baa ya Mbawala. Kijana Salim Hassan Mahoja na wenzake watatu wote wakiwa ni MAJANJAWIRI walitumika kushiriki uchomaji moto wa baa hiyo. Kwa kuwa mmiliki wa baa hiyo alijua kua vitendo vya fujo vingeweza kupelekea baa yake kuchomwa, aliomba ulinzi mapema kutoka katika jeshi la polisi.
Askari watatu waliokuwa na silaha bila ya sare walilala katika baa hiyo wakiwasubiri wahalifu pindipo baa hiyo ingevamiwa na kuchomwa. Vijana waliopangwa kuiripua baa hiyo Salim na wenzake walifika katika eneo la tukio usiku na kujaribu kutaka kuchoma moto baa hiyo kama walivyoagizwa. Bahati mbaya askari waliokuwa wamejificha ndani ya baa hiyo waliwashambulia kwa risasi za moto na kijana Salim akafariki hapo hapo huku vijana wenzake wawili wajeruhiwa kwa risasi.
Maiti na majeruhi wote wakapelekwa hospitali ya Mnazi mmoja. Jambo hili limefunkwa halikusemwa wala halikuripotiwa katika vyombo vya habari. Kwa michezo hii ni vipi tusiamini maskani ya KISONGE na nyengine hazikuchomwa kwa mipango hii michafu? Tutaamini vipi askari wa FFU hakuuliwa kwa mipango hii? Tutaamini vipi Sheikh Farid kiongozi wa UAMSHO hakutekwa na mipango hii?
Yote haya yanafanywa ili kuhalalisha hujuma na mateso dhidi ya wana CUF chini ya kisingizio kipya cha UAMSHO baada ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai kutangaza rasmi katika vyombo vya habari kwamba sasa anataka kupambana na adui yao mmoja mwenye sura mbili, yaani CUF na UAMSHO.
Safu ya Juu ya Uongozi katika hujumaKuthibitisha zaidi kuwa serikali ya Muungano na vibaraka wake wa Zanzibar hawana nia njema kwa Wazanzibari na kwamba wao bila shaka ndio wanaoandaa vitendo vya hujuma na vurugu vinavyoendelea Zanzibar ni kikao cha siri kilichofanywa baina ya Rais Kikwete na viongozi wenzake wa Jamhuri ya Muungano kwa upande mmoja na Rais wa Zanzibar na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa upande wa pili.
Kikao kilichoitwa ni cha kuzungumzia hali tete ya Zanzibar kilifanywa na viongozi wa SMT na SMZ huku wakimtenga Makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar akiwa ndio kiongozi wa pili kwa ukubwa katika serikali ya Zanzibar. Hii imefanywa kusudi ili kuhakikisha kuwa siri za mipango michafu na hujuma ianyotekelezwa Zanzibar haivuji na kufahamika na viongozi wa CUF kwa kuwa ni dhahiri mipango hiyo wao ndio inayowalenga.Dk. Shein na Kikwete tunakwambieni mufunguke na muache mara moja dhamira zenu mbaya kwa Zanzibar iliyokwisha kujifungua. Tumeugua maradhi ya kugombanishwa miaka mingi na mwisho tuliyapatia dawa. Baada ya kuyapatia dawa maradhi hayo wazanzibari tumefahamu tutakacho, na bila ya kutafuna maneno ni nchi yetu yenye mamlaka kamili.
Wazanzibari tumeapa hatuondoki katika mstari huo. Tunakutahadharisha sisi haturudi nyuma wala hatutetereki tunazidi kushikamana sote tunaohitaji mabadiliko kuelekea mamlaka kamili ya nchi yetu. Wimbi letu ni kubwa sana, nyinyi hamna uwezo wa kulizuia wala kulishinda. Anzeni kutafakari kabla ya hayajawakuta ya Mubarrak wa Misri itakapofika mwaka 2014 pale Wazanzibari tutakapopitisha maamuzi yetu ya Muungano wa MKATABA.

WANAFUNZI WA KIDATO CHA SITA WALIA


Wanafunzi kidato cha sita walia zanzibar

TAMKO LA KAMATI YA UTETEZI YA WANAFUNZI WA KIDATO CHA SITA DHIDI
MAMIA YA WANAFUNZI WA ZANZIBAR KUFUTIWA USAJILI WA MTIHANI (ACSEE 2013)
Wanafunzi kidacho cha sita walia Zanzibar kwa kufutiwa usajili wao wa kufanya mitihani

Wanafunzi kidacho cha sita walia Zanzibar kwa kufutiwa usajili wao wa kufanya mitihani
Ikiwa bado machozi hayajatukauka katika nyuso zetu kwa tukio la Mei mwaka huu baada ya maelfu ya wanafunzi wa Zanzibar kubatilishiwa matokeo yao ya somo la Dini “Islamic Knowledge” ya Kidato cha Sita kwa mwaka 2012 na linaloitwa Baraza la Mtihani Tanzania (NECTA) .
Aidha, ni miezi michache tu tangia kufutiwa kwa matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne(CSEE) mapema mwezi Februari mwaka huu ambapo wanafunzi 3,303 kati ya wanafunzi 450,324 waliofanya mtihani mwaka mwaka 2011 na kuifanya nchi yetu Zanzibar kuwa muhanga mkuu wa suala hili kwa zaidi ya shule ya 30 kufutiwa matokeo hayo ikwemo Shule ya Sekondari Mazizini, Hamamni, Mikumguni, Regeza Mwendo, Filter, Laureate, High View na nyingi nyenginezo.
Katika hali isyotarajiwa, mnamo tarehe 22/12/2012 Shule mbali mbali za sekondari hapa Zanzibar zilipokea barua yenye Tarehe 18/11/2011 kutoka Baraza la mtihani Tanzania (NECTA) zilizoorozesha majina mbali mbali ya wanafunzi ambao tayari walishatambuliwa usajili wao kabla na hatimae kubatiliwa usajili wao katika barua hizo.

Miongoni mwa shule zilizokumbwa na kadhia hio kwa Mkoa wa mjini Magharibi ni pamoja na Haile Sallasie (wanafunzi 56), Mwanakwerekwe “C” (36), Hamamni (35), Chukwani (15), K/samaki (12), Kiponda (11), Laureate (10) , Vikokotoni (3) na kwa upande wa Pemba ni Mchangamdogo (24) na CCK Kiuyu (8) na nyingi nyengine ambazo bado takwimu zake hatuzipata kwa wilaya mbali mbali Zanzibar , idadi hizi zinakamilisha jumla ya wanafunzi 215 waliofutiwa usajili huo kwa skuli hizi 11 tu.
Kwa mujibu wa barua hizo, wanafunzi hao wamezuiliwa usajili kwa kisingizio cha kutotimiza sifa za kuwa na alama 5 (5 PASSES) katika matokeo ya mitihani yao ya Form IV “Certificate of Secondary Education Examination “(CSEE) ukizingatia wanafunzi hao walitangazwa na kupangiwa shule mbali mbali na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar mnamo April mwaka 2011 na ambao walitarajiwa kufanya mtihani yao ya ACSEE mnamo February 2013.
Kwa masiktitiko na hudhuni kubwa, leo hii tunaletewa taarifa kuwa wanafunzi hawa hawana sifa za kufanya mtihani huo (ACSEE) katika kipindi ambacho tayari wameshakamilisha mashariti (conditions) yote muhimu ya mtihani huo ambapo ni pamoja na kulipia ada ya 45,000 Tsh (registration fee) na kufanya “project” na wamebakisha miezi 2 tu kufanya mitihani hiyo.
Kwa kuwa hali hii inakandamiza juhudi za serikali yetu tukufu katika kuendeleze na kukuza kiwango cha elimu pamoja na kupambana na Umasikini Zanzibar na vile vile kuhatarisha kushuka kwa kiwango cha wasomi nchini kwetu na hatimaye kudunisha maendeleo ya Zanzibar.
Kufuatia kadhia hii, Wanafunzi wa sekondari kutoka shule mbali mbali za Mkoa wa Mjini Magharibi ikwemo Hamamni, Haile Sallasie, Vikokotoni, Chukwani, Mwanakwerekwe “C”, Kiponda, na Lumumba tuliamua kukutana pamoja siku ya Jumamosi ya 25/11/2012 ili kuweza kuungana kupigania haki za wanafunzi wenzetu ambao kwa sasa wapo katika hali tatanishi.
Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na zaidi ya wanafunzi 70 ikiwa ni wawakilishi kutoka shule mbali mbali , tuliamua kuteau kamati maalumu kuweza kufanikisha utetezi wa suala hili ambayo iko chini ya ndugu Omar S. Omar (Mwanakwerekwe “C”) ambaye ni mweyekiti wa kamati hio akisaidiwa na Rahma Mbarak Shaali (Vikokotoni), makamo mwenyekiti wa kamati hio ya muda, naye ndugu Rashid Mohammed Rashid (Lumumba) alichaguliwa kuwa ni Msemaji wa Kamati hio pamoja na ndugu Saleh Abdallah Khatib (Haile Sallasie) alichaguliwa kuwa Katibu, zaidi ya viongozi hawa wane (4) kamati pia imeundwa na wajumbe wengine 8 ambao ni Said Bakar Said (Mwanakwerekwe “C”) , Seif Khamis Mbarouk (Vikokotoni), Aisha Moh’d khamis (Mwanakwerekwe “C”) , Mohammed Khatib Mohammed (K/samaki), Hamad Khamis Ahmed (Kiponda), Hassan Ally shee (Lumumba), Suleiman Juma Khamis (Kiponda), na Haji Ali Abdalla (Vikokotoni).
Kamati iliweza kuandaa maadhimio manne (4) ambayo yameweza kufikishwa katika sehemu husika ambayo ni haya yafuatayo , kwanza, ”Tunaitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo Ya Amali Zanzibar
(WEMA) kuhakikisha wanafunzi wote walofutiwa usajili wanasajiliwa na kufanya mitihani mnamo tarehe 08/02/2013 kama wanavyotarajiwa kufanya wanafunzi wengine”, Pili, ” wanafunzi wote wa Zanzibar wa Msingi na Sekondari kwa kitu kimoja kupinga uamuzi batili wa Baraza la mtihani Tanzania NECTA na kuwa tayari kuungana pamoja kutetea na kulalamikia kadhia hii katika ngazi zote zinazohusika” , Tatu, ”Kamati mbali mbali za wazazi za shule za Zanzibar na wazanzibar wote Unguja na Pemba kuwaunga mkono wanafunzi hawa katika kudai haki zao”, na Mwisho ni ”Tunawaasa Wanafunzi wote Zanzibar kuwa pamoja na kushiriki maandamano ya Amani yatakayoratibiwa na Kamati endapo tatizo hili halitopatiwa ufumbuzi kwa wakati stahiki”.

Katika kufanikisha maadhimio hayo Kamati imeweza kwa kushirikiana na vyombo mabli mbali vya habari kufikisha ujumbe huu kwa walengwa na wahusika , kamati iliweza kufanya vipindi cha moja kwa moja na vya habari kupitia Radio Nuru Fm, Hits Fm na Zenji FM, Tv Iman, Radio Iman, ZBC Tv na vyingi vyengine.
Kutokana na juhudi za kamati kutaka kuonana na Waziri wa Elimu Zanzibar kugongwa mwamba, kamati imeweze kupeleka barua rasmi katika wizara hio husika kulalamikia kadhia hio pia kamati imepeleka barua za malalamiko kwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.

Zaidi ya majibu aliotoa Katibu wa Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Kupitia kituo cha Zenji Fm radio tarehe 26/11/2012 kuwa watalifanyia kazi suala hili na majibu ya Waziri wa elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mh: Ali Juma Shamuhuna kwa kusema NECTA na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Haiwapi ushirikiano wa Kutosha katika baadhi ya maamuzi ya mambo yao hususani yanayoyohuisana na mitihani , vile vile na kauli ya Muheshimwa Makamo wa Kwanza wa Raisi Maalim Seif Sharif Hamad kuzitaka wizara mbili hizi za elimu kukaa pamoja kulitafutia ufumbuzi suala hili, aliyoyasema ofisi za wizara ya Elimu Mazizini Zanzibar mnamo 27/11/2012, Kamati bado haijapokea majibu yoyote rasmi kutoka sehemu husika na vile vile haijaridhishwa sana na majibu yaliyotolewa na hivo inasisitiza hatua za haraka kuchukuliwa.
Mwisho, Kamati inasiisitiza kuweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka kwa suala hili kwani huenda likaleta janga kubwa katika mustakabali mzima wa elimu katika nchi yetu ya Zanzibar


MSEMAJI MKUU WA KAMATI,
………………………….
RASHID MOH’D RASHID (LUMUMBA )

DOLE WATAKA SERIKALI MBILI


Dole wataka Serikali Mbili

dole
Katika ukusanyaji wa maoni kwa ajili ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye jimbo la Dole asubuhi ya tarehe 1 Disemba 2012, waliotaka mfumo wa Muungano huu uliopo kati ya Tanganyika na Zanzibar uendelee kama ulivyo bila ya kufanyiwa marekebisho ni 115 na waliotaka Zanzibar na Tanganyika ziwe na Muungano utakaoiwezesha Zanzibar kuwa na mamlaka yake kamili ikifuatiwa na Muungano wa mkataba ni 5.  Tume ya Kukusanya Maoni ya wananchi jioni ya leo itakuwa shehia ya Kinuni, wilaya ya Magharibi Unguja.