Kikwete, Shein mwaumbuka Zanzibar – Sehemu ya Kwanza
Maridhiano ya Wazanzibari hayakutoka Dodoma na kuna kila ushahidi kuwa hayakupata Baraka za Dodoma. Maridhiano ya Wazanzibari hayakutoka kwa wahafidhina, maagenti wa Dodoma walioko Zanzibar na halkadhalika kuna kila aina ya ushahidi sio tu hayakupata baraka zao lakini waliyapinga na wanaendelea kuyapinga kwa nguvu zao zote. Shabaha ya kupinga maridhiano ya Wazanzibari na serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kujenga farka, fitna, chuki, ukabila, ugozi, chokochoko na uvunjifu wa umoja na mshikamano miongoni mwa wazanzibari ili kurejesha hali kama ilivyokuwa huko nyuma. Lengo ni kwamba Dodoma (mkoloni mpya wa Zanzibar) aendelee kuitawala Zanzibar na mawakala wao (wahafidhina wa Zanzibar) waendelee kujaza matumbo yao huku wazanzibari walio wengi wakiteseka ndani ya ardhi yao tukufu.
Lengo kuu la mtandao huu wa kupinga maridhiano ni kujaribu mbinu
hii na ile ili kuizima nuru njema ya umoja wa wazanzibari ambayo ndio
silaha pekee wanayoitegemea hivi sasa katika kuirejesha Jamhuri ya watu
wa Zanzibar. Lengo ni lile lile linaliandaliwa na “system” chini ya
watawala wa Jamhuri ya Muungano na vibaraka wao wa Zazibar kuwa
wazanzibari wasambaratike, wagombane, wasiwe wamoja, wasiaminiane na
wasisikilizane.
Wanamtandao wanafahamu kwamba Wazanzibari wakiwa wamoja wanapata
jukwaa la pamoja la kujadili na kusahau mawazo ya tofauti zao za kisiasa
na huhisi machungu ya kudhalilika kwa nchi yao. Ukiwaondoa wazanzibari
katika maelewano na umoja kwa kujenga mazingira ya kila upande uone bado
sisi ni maadui kumbe baina yetu unafanikisha mpango wa kuwagawa katika
agenda tunayoipigania.Mbinu kubwa wanayotumia maadui hawa wa Zanzibar
hivi sasa ni ile ya kuandaa matukio mbali mbali na kuyanasibisha matukio
hayo na UAMSHO kwa upande mmoja na kwa upande wa pili wakifanya kila
wawezalo kuziunganisha harakati za UASHO na zile za chama cha CUF na
kuziundia harakati zote mbili picha ya uongo zionekane kuwa zipo chini
ya mwamvuli mooja na amri moja.
Lakini hebu tujiulize hivi hapa maadui hawa wa Zanzibar wamekuja na
staili mpya? Haya ni mambo makongwe kabisa kwa Zanzibar ambayo
yameshazoeleka. Kwa lugha nyengine hizi ni propaganda za kitoto kwa
wazanzibari, hakuna jipya.Siku ya tarehe 3 Machi 1996, enzi zile
wazanzibari walipogawanywa na kutiwa chuki baina yao ilidaiwa na
serikali kuwa mafiasa watatu wa usalama waliokuwa kwenye doria huko
katika kijiji cha Shengejuu, kisiwani Pemba, walipigwa na kuporwa silaha
na wanakijiji. Kwa sura ya kawaida ya uaskari ni vigumu kuaminika
kwamba askari watatu wakiwa na silaha mikononi waporwe silaha zao wote
watatu na wapigwe bila ya wao hata kujeruhi mtu yeyote au kujeruhiwa wao
wenyewe.
Muda sio mrefu, siku ya pili yake tu, kijiji hicho kilivamiwa na
kiasi cha askari wapatao 300 wa kikosi cha FFU na jeshi la wananchi
(JWTZ) waliokuwa wako kamili kivita. Unyama, mateso na vitendo vya
kihuni walifanyiwa wananchi wa kijiji cha Shengejuu. Sio tu unyama huo
walifanyiwa washukiwa, lakini pia mateso yaliwakuta watu wengi waliokuwa
hawana hatia yoyote. Baadhi ya wanakijiji walipigwa hadi kuzirai,
wengine waliibiwa mali zao kama vile kuku na mbuzi, maduka yaliporwa,
wanawake walibakwa na watu wapatao 80 waliwekwa ndani.
Kati ya watu hao 80, watu 30 waliachiliwa huru na waliobaki
waliendelea kusota ndani kwa kipindi kirefu sana. Kiongozi mmoja mkuu wa
SMZ wakati ule, aliwahi kufanya mkutano na waandishi wa habari kuelezea
hali ya mtafaruku inayoendelea katika kijiji hicho cha Shengejuu, na
hapa namnukuu moja ya kauli zake aliyoitoa kupitia kikao hicho“Sasa
tunataka kuwafanya watu wajue kama serikali ipo”.
Katika enzi hizo wafuasi wa CUF walikuwa wakisingiziwa kuhusika na
hujuma mbalimbali kama vile kuchomwa moto madarasa ya skuli, kupaka
vinyesi kwenye kuta za skuli, kutia vinyesi kwenye visima n.k. Hizi bila
shaka zilikuwa ni mwendelezo wa propaganda chafu za kisiasa zilizokuwa
na lengo la kujenga picha ya uongo na kuhalalisha hujuma dhidi ya watu
wasio na hatia. Waliokuwa wakifanya haya ni watu waliofundishwa vyema
propaganda na siasa chafu za uchochezi. Wakitekeleza vitendo hivyo huku
wakilindwa na askari polisi.
Madhumuni ni kuendelea kupata fursa ya kuwatesa raia wasio na hatia
kwa kuwapiga, kuwaweka gerezani na kuwaua. Waliokuwa wakifanya vitendo
hivyo hawakujua kwamba walikuwa wanaonekana na wanafuatiliwa nyendo zao
na hivyo kufahamika wao na waliowatuma.
Mkasa wa Shengejuu 1996
Katika hatua nyengine Siku moja wanakijiji hao hao wa Shengejuu
katika nyakati za usiku wakiwa katika doria yao ya kuangalia ni nani
hasa wanaofanya vitendo hivi, walifanikiwa kuwafumania watu hao. Wakiwa
wanaendelea na doria, wanakijiji hao waliiona gari yenye namba za
usajili ZNZ-12633 inayomilikiwa na usalama wa taifa ikisimama kiasi cha
umbali wa mita 100 hivi kutoka ilpokuwepo skuli ya Shengejuu (Soma
kitabu cha Dr. Mohamed Bakari, 2001 kiitwacho The Democratization
Process in Zanzibar).
Ghafla watu watatu waliokuwa na galoni la mafuta ya petroli
walishuka kutoka katika gari hiyo. Haraka haraka wakamwaga mafuta na
kuchoma baadhi ya majengo ya shule hiyo na kukimbia. Wanakijiji
wakajitokeza ghafla na kuwazingira wahalifu hao. Lakini mara milio ya
risasi hewani ikasikika na watu hao kuingia ndani ya gari yao na
kukimbia. Wanakijiji waliwahi kuuzima moto huo. Ilithibitika kuwa watu
waliofanya vitendo hivyo ni wanamaskani waliokuwa wakilindwa na
wanausalama ndio waliokuwa wakitekeleza vitendo na hujuma zile kwa nia
ya kukizulia chama cha CUF na kuwatesa raia bila ya hatia yoyote kwa
maslahi binafsi ya kisiasa.
Wimbi la Mageuzi Zanzibar lawatisha wahafidhina na watawalaMaadui
wa Zanzibar baada kuliona wimbi la kudai mabadiliko katika mfumo na
muundo wa Muungano wa Tanzania linaongezeka wameamua kujipanga upya na
kujaribu kuwasambaratisha wazanzibari ili wasifikie lengo lao kwa
kupitia mbinu hizo zilizotumika huko nyuma za kuandaa uongo na
kuupandikiza katika jamii. Bila shaka wakitarajia uongo huo utaweza
kuzaa chuki na fitna miongoni mwa makundi mabali mbali yaliyoshika kamba
ya pamoja kutafuta maslahi ya nchi yao na hivyo kuiwachia kamba hiyo na
kusambaratika.
Chuki ambazo zinajengwa hapa ni baina ya CUF na CCM kwa vitendo
kama vile vya kuzichoma moto maskani za CCM na kuwasingizia CUF.
Kuwatesa wafuasi wa CUF kwa visingizio mbali mbali kama vile kupambana
na UAMSHO ili wafuasi wa CUF wakasirike na serikali na chao kwa kuwa CUF
ni sehemu ya serikali hiyo. Wafuasi wa CUF wakikasirika dhidi ya chama
chao itakuwa tayari umefanikisha kulisambaratisha kundi kubwa
linashikilia engine ya kudai mabadiliko na hivyo kuliwacha kundi hilo
likiwa dhaifu.Maadui hawa wa Zanzibar wameunda makundi maalum ya
uharamia kama vile Ubaya Ubaya, Mbwa Mwitu na mengineyo. Makundi yote
hayo yakitoka katika kundi kuu la awali la MAJANJAWIRI. Inaeleweka
kwamba janjawiri ni vijana waliochukuiwa kutoka katika maskani za CCM na
kupewa mafunzo ya kiaskari kwa lengo la kuajiriwa katika vikosi vya
SMZ.
Baada ya kukosa ajira vijana hawa hupewa ajira ya muda ya kufanya
hujuma mbali mbali ili kutimiza maslahi binafsi ya chama cha CCM. Hivi
sasa majanjawiri wakiwa katika vikosi vipya vya ubaya ubaya na mbwa
mwitu wamekuwa wakiratibu na kutekeleza vurugu barabarani, kuchoma moto
matairi, na kuchoma moto maskani na makanisa. Halkadhalika vijana hawa
ambao ni wepesi wa kuuwa ndio wanaotumika kufanya mauwaji na kisingiziwa
vijana wa UAMSHO.Mkasa wa Baa ya Mbawala 2012
Kuna taarifa za uhakika za kikao cha CCM mkoa wa Mjini magharibi
kilichosimamiwa na mwenyekiti wake Borafia Silima cha kupanga hujuma za
uchomwaji moto wa baa ya Mbawala. Kijana Salim Hassan Mahoja na wenzake
watatu wote wakiwa ni MAJANJAWIRI walitumika kushiriki uchomaji moto wa
baa hiyo. Kwa kuwa mmiliki wa baa hiyo alijua kua vitendo vya fujo
vingeweza kupelekea baa yake kuchomwa, aliomba ulinzi mapema kutoka
katika jeshi la polisi.
Askari watatu waliokuwa na silaha bila ya sare walilala katika baa
hiyo wakiwasubiri wahalifu pindipo baa hiyo ingevamiwa na kuchomwa.
Vijana waliopangwa kuiripua baa hiyo Salim na wenzake walifika katika
eneo la tukio usiku na kujaribu kutaka kuchoma moto baa hiyo kama
walivyoagizwa. Bahati mbaya askari waliokuwa wamejificha ndani ya baa
hiyo waliwashambulia kwa risasi za moto na kijana Salim akafariki hapo
hapo huku vijana wenzake wawili wajeruhiwa kwa risasi.
Maiti na majeruhi wote wakapelekwa hospitali ya Mnazi mmoja. Jambo
hili limefunkwa halikusemwa wala halikuripotiwa katika vyombo vya
habari. Kwa michezo hii ni vipi tusiamini maskani ya KISONGE na nyengine
hazikuchomwa kwa mipango hii michafu? Tutaamini vipi askari wa FFU
hakuuliwa kwa mipango hii? Tutaamini vipi Sheikh Farid kiongozi wa
UAMSHO hakutekwa na mipango hii?
Yote haya yanafanywa ili kuhalalisha hujuma na mateso dhidi ya wana
CUF chini ya kisingizio kipya cha UAMSHO baada ya Naibu Katibu Mkuu wa
CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai kutangaza rasmi katika vyombo vya habari
kwamba sasa anataka kupambana na adui yao mmoja mwenye sura mbili, yaani
CUF na UAMSHO.
Safu ya Juu ya Uongozi katika hujumaKuthibitisha
zaidi kuwa serikali ya Muungano na vibaraka wake wa Zanzibar hawana nia
njema kwa Wazanzibari na kwamba wao bila shaka ndio wanaoandaa vitendo
vya hujuma na vurugu vinavyoendelea Zanzibar ni kikao cha siri
kilichofanywa baina ya Rais Kikwete na viongozi wenzake wa Jamhuri ya
Muungano kwa upande mmoja na Rais wa Zanzibar na Makamo wa Pili wa Rais
wa Zanzibar kwa upande wa pili.
Kikao kilichoitwa ni cha kuzungumzia hali tete ya Zanzibar
kilifanywa na viongozi wa SMT na SMZ huku wakimtenga Makamo wa kwanza wa
Rais wa Zanzibar akiwa ndio kiongozi wa pili kwa ukubwa katika serikali
ya Zanzibar. Hii imefanywa kusudi ili kuhakikisha kuwa siri za mipango
michafu na hujuma ianyotekelezwa Zanzibar haivuji na kufahamika na
viongozi wa CUF kwa kuwa ni dhahiri mipango hiyo wao ndio
inayowalenga.Dk. Shein na Kikwete tunakwambieni mufunguke na muache mara
moja dhamira zenu mbaya kwa Zanzibar iliyokwisha kujifungua. Tumeugua
maradhi ya kugombanishwa miaka mingi na mwisho tuliyapatia dawa. Baada
ya kuyapatia dawa maradhi hayo wazanzibari tumefahamu tutakacho, na bila
ya kutafuna maneno ni nchi yetu yenye mamlaka kamili.
Wazanzibari tumeapa hatuondoki katika mstari huo.
Tunakutahadharisha sisi haturudi nyuma wala hatutetereki tunazidi
kushikamana sote tunaohitaji mabadiliko kuelekea mamlaka kamili ya nchi
yetu. Wimbi letu ni kubwa sana, nyinyi hamna uwezo wa kulizuia wala
kulishinda. Anzeni kutafakari kabla ya hayajawakuta ya Mubarrak wa Misri
itakapofika mwaka 2014 pale Wazanzibari tutakapopitisha maamuzi yetu ya
Muungano wa MKATABA.
No comments:
Post a Comment