Viongozi wa kijadi kaskazini mwa
Ghana wamekubaliana kumaliza vitendo vya mauaji ya watoto wachanga
wenye ulemavu ambao inaaminika walikuwa na pepo.
Watoto wenye ulemavu walionekana kama wenye mkosi hivyo walinyweshwa sumu ili kuwaua.
Mmoja wa wanaharakati ameiambia BBC kwamba, kuboreshwa kwa huduma za afya na elimu kumesababisha kupungua kwa imani hizo potofu.
Mwanaharakati Raymond Ayine, amepongeza uamuzi
huo ambao utahusisha miji saba. Lakini akadai kwamba, hakuna uhakika
kama mauaji hayo yamezuiwa nchi nzima.
Mwandishi wa BBC, Vera Kwakofi, anasema mkoa wa
Kasena Nankana ambako uamuzi huo umetangazwa ni eneo ambalo imani hiyo
ilikuwa imeshamiri.
Wakati mwingine watoto waliozaliwa na kuhisiwa
kuwa ni mkosi katika familia pia walituhumiwa kuwa watoto wenye mapepo
nao waliuawa.
Kundi la wanaume waliokuwa wakiwapa sumu watoto,
sasa wamepewa majukumu mapya ambapo watafanya kazi na watoto hao
walemavu kuhamasisha haki zao.
Mwandishi mmoja wa habari za kiuchunguzi, Anas
Aremeyaw, ameiambia BBC kwamba, alichukua mwanasesere na kumpeleka kwa
mtabiri, na kumwambia kuwa huyo alikuwa mtoto mwenye matatizo ya kula
chakula na ulemavu wa viungo.
Baada ya mtabiri huyo kuzungumza na mizimu huku
akiruka juu na chini, na baada ya hapo alidai kwamba, mizimu
imethibitisha kwamba, mtoto huyo ana mapepo na anastahili kuuawa mara
moja na pia mtoto huyo tayari amekwishawaua watu wawili wa familia yake.
Mmoja wa viongozi wa kijadi, Naba Henry Abawine
Amenga Etigo, amesema kuwa, kuanzia sasa mtu yeyote atakayekamatwa
akijaribu kuwadhuru tena watoto wenye ulemavu atakabidhiwa kwa polisi.
Bwana Ayine, kutoka kundi la wanaharakati la
Afrikids, amesema amesikitishwa kwamba, katika zama hizi, mtoto anaweza
kupoteza maisha yake kwa sababu ya vitendo hivi vya kikatili.
Amebainisha kuwa, katika maeneo ya vijijini
ambako imani hizo zimeenea, wanawake kwa kawaida hujifungua bila kupata
huduma za wauguzi na hata vipimo kabla ya kujifungua. Kutokana na hali
hiyo, akina mama wajawazito hupata matatizo wakati wa kujifungua kuliko
sehemu nyingine.
Amefafanua kuwa, hata kabla ya mauaji hayo
kupigwa marufuku rasmi, hakukuwa na takwimu zilizohifadhiwa kuhusu
mauaji ya watoto wenye pepo katika eneo hilo katika kipindi cha miaka
mitatu iliyopita.
Katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Ghana,
wanawake vikongwe wanaotuhumiwa kwa uchawi, wakati mwingine hulazimika
kuhama makazi yao na kwenda kuishi kwenye kambi rasmi za watu
wanaotuhumiwa kwa uchawi.