Nambari hiyo haijatumika kwa zaidi ya miaka 15
Polisi nchini Kenya wameambia
BBC kuwa nambari ya kupiga wakati wa dharura 999 imeanza tena kutumika
baada ya miaka 15 ingawa watu wanapiga simu za utani.
Mwezi Julai mahakama iliamua kuwa polisi
werejeshe huduma hiyo mwishoni mwa mwezi Julai, lakini BBC ilipojaribu
kupiga simu hiyo haijibiwi kamwe.
Polisi walilazimika kufunga huduma hiyo mwaka 1998, kwa kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya wananchi.
Wenyeji walilazimika kupiga nambari za simu ambazo zilikuwa ndefu sana kuweza kupata huduma za polisi wakati wa dhahrura.
Ilikuwa bora kwa wenyeji kwenda kwa kituo cha
polisi kupata huduma walizohitaji au kuripoti kisa cha uhalifu kuliko
kupiga simu kutaka kusaidiwa na polisi.
Mkuu wa polisi mjini Nairobi Benson Kibui
aliambia BBC kuwa tangu nambari hii kuanza kutumika tena , watu wamekuwa
wakipiga simu za utani wakijidai kutafuta hoteli.
Pia kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa wanajaribu kuona ikiwa inafanya kazi.
Mwanaharakati wa Kenya Okiyo Omtatah alikwenda mahakamani akitaka nambari hiyo kuanza kutumika tena .