WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imeeleza kuwa
sekta ya uvuvi hivi sasa imezidi kuimarika baada ya wananchi wengi
kushajiika na kuanza kufuga mazao ya baharini kwenye maeneo yao
wanayoishi. Aidha, Wizara hiyo ilieleza kuwa uzalishaji wa mwani
umeongezeka kutoka tani 12,516 mwaka 2010 mpaka tani 13,040 mwaka 2011
ikiwa ni ongezeko la asilimia 4 na kuelezea mafanikio zaidi katika sekta
ya uvuvi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa shughuli za ufugaji wa
viumbe vya baharini kama vile samaki, kaa, kasa, majongoo na chaza.
Maelezo hayo yametolewa na uongozi wa Wizara hiyo, wakati wa mkutano
kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika kuangalia utekelezaji wa Malengo
Makuu ya Wizara hiyo kwa kipindi cha Aprili- Juni 2011-2012 na Julai-
Septemba 2012-2013. Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar
ambapo pia, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi
Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee alishiriki kikamilifu, Wizara hiyo ilieleza
kuwa mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa umeongezeka kutoka
asilimia 6.1 mwaka 2010 hadi 6.7 mwaka 2011.Akisoma taarifa ya utangulizi ya utekelezaji wa Malengo makuu hayo ya Wizara, Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdilahi Jihad Hassan alisema kuwa kiwango cha uvuvi wa samaki kimeongezeka kutoka tani 25,693 mwaka 2010 na kufikia tani 28,759 mwaka 2011 ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.6. Pia, Waziri Jihadi alieleza mafanikio mengine katika Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuanzisha mabwa mawili ya mfano ya kufugia samaki katika maeneo ya kiungoni na Pujini Pemba kama ni mashamba darasa kwa wafugaji wa samaki.
Kuongezeka kwa idadi ya samaki kulikotokana na kuimarisha usimamizi kwa maeneo ya hifadhi na kuendelea kutoa elimu kwa wavuvi pamoja na kuongezeka kwa taaluma juu ya athari ya matumizi ya mitego haramu na njia haramu za uvuvi. Pamoja na hayo, Wizara hiyo ilieleza mafanikiokatika sekta ya mifugo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mwamko wa ufugaji wa ngombe na mbuzi wa maziwa na kuku wa kienyeji ambapo jumla ya shamba darasa 180 za mbuzi wa maziwa, ngombe wa maziwa na kuku zimefanywa.
Uongozi huo pia, ulieleza kuwa Wizara imeandaa mipango kwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 ambapo miongoni mwa vipaumbele ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari, kutoa nafasi za ajira kwa vijana kupitia shughuli za ufugaji na uvuvi na kufanya utafiti juu ya maradhi ya mifugo. Akitaja miongoni mwa changamoto zilizomo katika sekta ya mifugo na uvuvi, Waziri Jihadi alisema kuwa nia pamoja na uhaba wa wataalamu wa fani ya ufugaji wa mazao ya bahari ambapo hivi sasa Wizara imo katika juhudi za kuwasomesha wafanyakazi katika Chuo cha Mbegani na tayari baadhi yao wamepekwa nchini India, China na Korea.
Uharibifu wa makaazi ya samaki unaosababishwa na matumizi ya uvuvi haramu wa nyavu za macho madogo, nyavu za kukokota na mfumo mbaya wa mitego inayobuniwa na wavuvi, ambapo tayari Wizara imeanzisha doria pamoja na kutoa elimu kwa wavuvi. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein pia, alikutana na uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na kuelezea utekelezaji wa Malengo Makuu ya Wizara hiyo kwa kipindi cha Aprili- Juni 2011-2012 na Julai- Septemba 2012-2013.
Ukitoa maelezo yake hayo, uongozi wa Wizara hiyo chini ya Waziri wake Mhe. Rashid Seif Suleiman, ulieleza kuwa imeendelea kutekeleza majukumu yake ya kusimamia maendeleo ya sekta ya usafiri na mawasiliano kwa kufuata muongozo wa bajeti ya Serikali unaosisitiza utekeleza wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA II), pamoja na maelekezo ya Rais. Waziri Suleiman alieleza kuwa Wizara yake imeweka vipaumbele katika kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na bandari pamoja na uimarishaji wa huduma za mawasiliano.
Alisisitiza kuwa utekelezaji wa vipaumbele hivyo unaendana na utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA II 2010-2015) ambayo pia, yamezingatia Dira ya maendeleo ya Karne ya 2020. Pamoja na hayo, Wizara hiyo ilieleza kuwa kazi ya uwekaji wa kifusi kwa tabaka la mwisho pamoja na matayarisho ya uwekaji wa lami ya maji zimefanyika katika barabara za Wete-Konde yenye kimolita 15.1 na barabara ya Wete-Gando yenye urefu wa kilomita 13.6.
Aidha, Wizara hiyo ilieleza kuwa kazi za matayarisho ya ujenzi ikiwemo upimaji wa eneo la ujenzi wa barabara za Koani-Jumbi yenye urefu wa kilomita 6.3 na Jendele- Cheju-Kaebona yenye urefu wa kilomita 11.7 zimefanyika. Akitoa maelezo yake kwa njakati tofauti alipokutana na viongozi na watendaji wa Wizara hizo, Dk. Shein alitoa pongezi zake kwa juhudi kubwa zilizochukuliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kusisitiza kuwa mafanikio waliyoyapata yametokana na mashirikiano makubwa waliyonayo.
Kutokana na hatua hiyo, Dk. Shein aliutaka uongozi huo kuongeza ushirikiano wao ili waweze kupata mafanikio makubwa zaidi katika utendaji wa kazi zao na hatimae kuendelea kuletea maendeleo nchini huku akipongeza jinsi Wizara hiyo ilivyowasilisha Bangokitita lake kwa ustadi mzuri. Pamoja na hayo, Dk. Shein alipokutana na uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano alipongeza juhudi inazozichukua Wizara hiyo katika kutekeleza kazi zake kwa upande wa Unguja na Pemba.
Stori na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
No comments:
Post a Comment