Kazi ya kutoa huduma ya barua-pepe kwa watumiaji milioni moja wa simu
za mkononi imekamilika, maafisa wa kampuni ya Telesom ya Somaliland
wameiambia Sabahi.
Telesom inajitayarisha kuzindua huduma hiyo iliyokuwa imesubiriwa kwa
muda mrefu wiki chache zijazo baada ya kuingia ubia na kampuni ya
kimataifa ya Kimarekani inayojihusisha na shirika ya kimataifa ya tovuti
na programu za kompyuta, Google, kutoa teknolojia hiyo, alisema mkuu wa
idara ya kimataifa ya Telesom, Mohamud Haji Abdirahman.
Telesom iliingia kwenye ubia na Google hapo Aprili 2011 kutoa huduma
hiyo mpya, ambayo itawaruhusu watumiaji wa Google kuwasiliana na wateja
wa Telesom bure kupitia ujumbe mfupi wa maneno wa simu za mkononi.
Mwezi uliopita, mwakilishi wa Google kwa nchi za Afrika chini ya
Jangwa la Sahara, Divan Lan, alivifanyia uchunguzi vifaa vya Telesom
katika makao makuu ya kampuni hiyo, mjini Hargeisa, kabla ya uzinduzi
huo.
Katika makubaliano ya ushirikiano wao, watumiaji wa Gmail wataweza
kutuma barua pepe kwa nambari za simu za mkononi za Telesom ambazo
zitawafikiwa watumiaji wa Telesom kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno,
alisema Abdirahman. Watumiaji hao wa simu nao wataweza kuzijibu barua
hizo kwa kutumia ujumbe mfupi wa maneno.
Abdirahman alisema kuzigeuza barua pepe kuwa ujumbe mfupi wa
maandishi kutawaruhusu watumiaji wa Telesom kuweza kutumia fursa za
mtandao wa Intaneti kuwasiliana kwa ufanisi zaidi.
Jambo hili linawaweka huru watu kutoka ile dhiki ya kutafuta migahawa
ya intaneti ambapo si kila mara hukuta kompyuta ya kutumia,” alisema.
“Kwa huduma hii sasa, watumiaji wataweza kujibu haraka ujumbe
wanaotumiwa kwa sababu wanaweza kuchukuwa simu popote pale.”
Huduma hii itakuwa na athari kubwa juu ya namna watu wanavyowasiliana
kwa kazi na kwa burudani, alisema Abdi Osman Ali, mtaalamu wa
teknolojia ya habari mjini Hargeisa. “Inaonesha maendeleo ambayo
Somaliland imeweza kuyafikia katika eneo la [teknolojia ya]
mawasiliano,” alisema.
Ubia wa Telesom na Google ni muhimu kwa sababu ambazo ziko juu ya
zile za utumaji wa ujumbe wa maandishi kwa barua pepe, kwa mujibu wa
mchumi, Abdirahman Aden Ismail.
Ismail anasema makubaliano hayo ni muhimu sana kwa sababu
yanatengeneza kigezo kwa makampuni mengine makubwa ya kimataifa kuwekeza
Somaliland. “Yanaweza kupelekea ubia wa Telesom na makampuni mengine
makubwa ya kimataifa,” Ismail aliiambia Sabahi.
Telesom iliundwa mwaka 2001 na kundi la Wasomali, baadhi yao
wanaoishi nje ya nchi, ili kutoa huduma pana zaidi za mawasiliano kwa
watumiaji kwenye eneo hilo.
Abdirahman alisema kampuni hiyo ilikuwa ya kwanza kutoa huduma za
simu ya mkononi nchini Somalia, ambayo inawawezesha wateja kutumia
huduma ya kuhamishia simu zao wanapokuwa nje, miongoni mwa mambo
mengine.
Mwaka jana, kampuni hiyo ilianzisha mtandao wa 3G huko Somaliland na
sasa inawahudumia zaidi ya wakaazi milioni moja wa Somaliland, alisema.
Kampuni hiyo inatarajia kushirikiana tena na Google kuanzisha huduma
za kuinua uchumi na hasa kushughulikia mahitaji ya sekta binafsi,
alisema.
No comments:
Post a Comment