Wednesday, August 14, 2013

Keita ashinda uchaguzi wa urais Mali


Ibrahim Boubacar Keita ana jazi ngumu ya kukarabati nchi ya Mali
Ibrahim Boubacar Keita ameibuka mshindi wa uchaguzi mkuu nchini Mali huku mpinzani wake akikubali kushindwa katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais.
Soumaila Cisse,amekubali kushindwa na mpinzani wake,aliyekuwa waziri mkuu Ibrahim Boubakar Keita.
Bwana Cisse aliyewahi kuhudumu kama waziri wa fedha amempongeza Keita kwa ushindi huo na kumtakia kila la kheri.
Bwana Keita, mwenye umri wa miaka 68, alihudumu kama waziri mkuu kutoka mwaka 1994 hadi 2000.
Mali imekumbwa na vurugu kwa kipindi cha mwaka mmoja ikiwemo mapinduzi ya kijeshi na kufuatiwa na harakati za jeshi la Ufaransa kuwaondoa wapiganaji waliokuwa wameteka eneo la Kaskazini mwa nchi.
Hata hivyo hakuna matokeo rasmi yametolewa kufuatia duru ya pili ya uchaguzi iliyofanyika Jumapili.
Katika duru ya kwanza bwana Cisse alipata 19% dhidi ya bwana Keita aliyepata 40%
Bwana Keita anayejulikana kama (IBK) - atakuwa na jukumu la kusimamia zaidi ya dola bilioni 4 za msaada wa kigeni kwa taifa hilo ambalo uliahidiwa kwa ukarabati wa nchi.
Umoja wa mataifa umeanza kupeleka kikosi cha wanajeshi 12,600 kitakachokuwa na jukumu la kudhibiti hali nchini Mali, huku wanajeshi wa Ufaransa wakianza kuondoka.
Baada ya duru ya kwanza ya uchaguzi Bwana Cisse alikuwa amelalamika kuwepo visa vya rushwa au ununuzi wa kura huku kura zaidi ya laki nne zikisemekana kuharibika.
Hata hivyo, mahakama ya kikatiba ya Mali ilikataa madai hayo huku kiongozi wa waangalizi wa Ulaya Louis Michel, akisifu uchaguzi huo kwa ulivyoandeshwa kwa njia ya uwazi.
Mnamo Jumatatu, waangalizi kutoka Muungano wa ulaya na muungano wa Afrika, walisifu ambavyo duru ya pili ya uchaguzi ilivyoendeshwa.
'Raia wa Mali wanapaswa kupongezwa kwa sababu kulingana na mimi ninavyoona, wanatii demokrasia,'' alisema Michel.
Kabla ya uchaguzi huo Bwana keita aliahidi kuleta maridhiano nchini humo iwapo angechaguliwa.
Makubaliano yaliyoafikiwa ili kuruhusu uchaguzi kuendelea katika eneo hilo la kazkazini yanashinikiza serikali iliyochaguliwa kuanzisha mazungumzo ya amani na waasi wa kundi la Tuareg katika kipindi cha miezi miwili.

No comments:

Post a Comment