Friday, December 28, 2012

Al-Shabaab yajikusanya upya huko Bulo Burde kabla ya shambulio kubwa


Na Majid Ahmed, Mogadishu

Desemba 27, 2012


Al-Shabaab wanajaribu kujikusanya huko mkoa wa Hiran wa Somalia baada ya kukabiliwa na mfululizo wa kushindwa na kupoteza miji ya kimkakati mmoja baada ya mwengine katika miezi ya hivi karibuni, maafisa wa usalama wa Somalia wasema.
  • Askari wa Jeshi la Taifa la Somalia wakiwa wamepumzika kwenye kivuli cha mti huko Jowhar tarehe 11 Disemba baada ya kuukamata mji uliokuwa unashikiliwa na al-Shabaab kwa msaada wa majeshi ya Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia. [Na Stuart Price/AU-UN IST/AFP] Askari wa Jeshi la Taifa la Somalia wakiwa wamepumzika kwenye kivuli cha mti huko Jowhar tarehe 11 Disemba baada ya kuukamata mji uliokuwa unashikiliwa na al-Shabaab kwa msaada wa majeshi ya Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia. [Na Stuart Price/AU-UN IST/AFP]
Ahmed Abdullahi, afisa wa usalama katika mkoa wa Hiran, alisema kuwa alipokea habari ya harakati ya baadhi ya viongozi wakuu wa al-Shabaab wanatoroka kutoka maeneo yaliyokombolewa na kuelekea Bulo Burde.
"Kwa mujibu wa kile ambacho tumeambiwa na wakaazi wa Bulo Burde baadhi ya viongozi wa al-Shabaab kama vile Yusuf Sheikh Isse, amabaye ni dhamana wa mkoa wa Shabelle ya Kati, na viongozi wengine wamekuwa wakija mji huu," Abdullahi aliiambia Sabahi.
"Tangu vikosi vya washirika vilipoukamata mji wa Jowhar, makamanda wa vita wa kikundi hicho wamekuwa wakiondoka kutoka maeneo ya Shabelle ya Kati na kuelekea Hiran ya mashariki," alisema na kuongeza kuwa vikosi vya Somalia na Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) vinajitayarisha kuelekea Bulo Burde.
"Jeshi la Taifa la Somalia, kwa msaada wa vikosi vya AMISOM, vimekuwa katika tahadhari na viko tayari kuikomboa miji michache iliyobakia katika makucha ya al-Shabaab, ikiwemo Bulo Burde," alisema.
Bulo Burde, ambao uko kilomita 240 kaskazini ya Mogadishu na kilomita 40 kusini mashariki ya Beledweyne, inachukuliwa kuwa ni ngome ya mwisho imara ya al-Shabaab huko Hiran.
Kwa mujibu wa wakaazi, mamia ya wapiganaji wa al-Shabaab wamejificha mjini humo, wakijitayarisha kuukinga baada ya kupoteza udhibiti wa miji mingi ya maeneo ya kusini na kati ya nchi.
Kikundi hicho cha wanamgambo kilitangaza wiki iliyopita kuwa kimeunda kikosi kimoja kipya kinachojulikana "Kikosi cha Abu Yahya al-Libi", kinachoitwa hivyo kwa jina la kiongozi wa al-Qaida ambaye iliripotiwa kuwa aliuliwa mapema mwaka huu huko Pakistani.
Tarehe 17 Disemba, al-Shabaab iliwaonesha wanachama wa kikosi hicho kipya katika shughuli iliyofanyika huko Bulo Burde kama juhudi za kuwapanga upya wapiganaji wake walioshindwa, kwa mujibu wa taarifa za habari.
Hata hivyo, jaribio la al-Shabaab kujikusanya upya linakabiliwa na vikwazo vingi kutokana na mizozo ya ndani inayoendelea baina ya uongozi wa al-Shabaab pamoja na matatizo ya kifedha ya kikundi hicho, wachambuzi wa masuala ya usalama wasema.
"Al-Shabaab imepoteza maeneo ya kimkakati ambayo yalikuwa yakileta mapato kama vile Mogadishu na Kismayu, kwa hivyo haitaweza kupata fedha za kutosha kujipanga yenyewe na kugharamia operesheni zake za kijeshi," alisema Mohamed Ali Mohamed, kepteni mstaafu wa Idara Usalama wa Taifa la Somalia.
Al-Shabaab haitaweza kulinda Bulo Burde, Mohamed alisema. Kinyume chake, wapiganaji watarudi nyuma na kuelekea misituni baina ya mikoa ya Shabelle ya Kati na Hiran kwa ajili ya kujikinga, alisema.
"Kama ambavyo tulivyoona katika miezi iliyopita, wapiganaji wa al-Shabaab wamekuwa wakirejea nyuma kutoka miji yote bila ya ushindani mara tu vikosi vya washirika vinapokaribia," aliiambia Sabahi.
"Kujitoa kwa Al-Shabaab kutoka miji ya kimkakati kuelekea maeneo ya vijijini hakumaanishi kuwa wamechagua kutojihusisha na vita ili kuepuka kupata hasara kubwa," alisema. Maana yake ni kwamba kikundi hakiwezi kuhimili mashambulizi na kuyakinga maeneo yaliyo katika udhibiti wao, kwa hivyo wanachama wake hukimbilia maeneo ya vijijini kwa kujilinda."

Al-Shabaab inawalazimisha watoto kubeba silaha

Wakaazi wa eneo la Bulo Burde walisema kwamba al-Shabaab imewateka nyara watoto na kuwalazimisha kubeba silaha katika juhudi ya kukinga mashambulizi kutoka Jeshi la taifa la Somalia na majeshi ya AMISOM.
"Al-Shabaab imewakamata watoto wasiopungua 150 kutoka shule na madrasa ya Qur'an ambao wametekwa kutoka kote nchini na vijiji vidogo vinavyoizunguka Bulo Burde," mkaazi Abdinur Dahir mwenye umri wa miaka 46, aliiambia Sabahi.
"Viongozi wa al-Shabaab akiwemo Sheikh Yusuf Ali Ugas, afisa wa kikundi hicho katika mkoa wa Hiran region, pamoja na viongozi wengine sasa wapo mjini," alisema. "Wanawataka walimu katika shule za Qur'an na shule za kawaida kusitisha masomo yao na kuwapeleka wanafunzi wao kwenye kambi za mafunzo ili waweze kujifunza jinsi ya kutumia silaha na kujiunga na kikundi hicho katika vita vyake vya jihadi, kama wanavyodai."
Nasra Abdi, mwenye umri wa miaka 42, anayeuza maziwa safi katika soko la mji, alisema aliwaona wanachama wa al-Shabaab mitaani, wakiwataka wakaazi kujiunga na kikundi hicho ili kuulinda mji dhidi ya shambulio linalotarajiwa kutoka vikosi vya Somalia na washirika.
"Kikundi hiki ni adui wa watu wa Somalia kwa sababu ya vitendo vyao dhidi ya watu wasio na hatia, hasa vijana ambao wanalazimishwa kubeba silaha na kupigana kwa ajili hao," alisema.

No comments:

Post a Comment