Monday, December 10, 2012

Majambazi yapora mradi wa maji Z’bar



Majambazi yamevamia kituo cha mradi wa maji vijijini na kuiba fedha taslim Shilingi milioni tisa na vifaa mbalimbali katika kijiji cha Kiashange Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Majambazi hao walivamia kituo hicho juzi wakiwa katika gari mbili aina Escudo.
Mbali ya fedha taslim, pia waliiba kompyuta za mkononi mbili, mashine za DVD mbili, simu za mkononi saba na kamera za mradi huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar, (Zawa) kuimarisha ulinzi katika miradi ya maendeleo kama hiyo.
Alisema wakati umefika kwa Zawa kuhakikisha walinzi wenye sifa ndiyo wanapewa dhamana ya kulinda miradi mikubwa wakiwa na silaha za moto badala ya kuweka askari wa korokoroni wakiwa na virungu.
Balozi Seif alitoa agizo hilo wakati akiwapa pole watendaji wa kituo hicho cha mradi maji safi vijijini.
Alisema kutokana na mabadiliko ya dunia, ipo haja ya kuimarishwa zaidi ulinzi wa uhakika na kuachana mfumo wa ulinzi wa kutumia virungu ambavyo vimepitwa na wakati hasa katika miradi mikubwa inayofadhiliwa na wafadhili ukiwamo mradi huo.
Aidha, Balozi Seif alivitaka vyombo vya ulinzi kuwasaka majambazi hao mpaka wapatikane na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Awali Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (Awa), Dk. Mustafa Ali Garu, alisema mradi wa maji safi vijijini wa Kiachange ni miongoni mwa miradi mikubwa mitatu inayotarajia kutumia dola milioni 47 za Marekani chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Mradi huo pia utasadia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Mkoa wa mjini Magharibi na kisiwani Pemba ambapo SMZ itachangia asilimia 10 ya gharama za ufanikishaji wa mradi huo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment