Friday, December 28, 2012

Mjadala waendelea kuhusu dhima ya serikali ya muungano nchini Tanzania


Na Deodatus Balile, Dar es Salaam

Dhima na muundo wa serikali ya muungano kwa mara nyingine tena vimechochea mjadala mkali miongoni mwa Watanzania wakati Tume ya Kupitia upya Katiba (CRC) ilifanya mfuatano wa mikutano na wananchi huko Zanzibar wiki iliyopita.
  • Rais wa visiwa vinavyojitawala kwa sehemu vya Tanzania Zanzibar Ali Mohamed Shein (kulia) akisalimiana na rais wa Tanzania Jakaya Kikwete wakati wa sherehe za Kikwete kuapishwa jijini Dar es Salaam tarehe 6 Novemba 2010. Zanzibar iliungana na Tanganyika bara mwaka 1964, na kuunda Tanzania. [Yasiyoshi Chiba/AFP] Rais wa visiwa vinavyojitawala kwa sehemu vya Tanzania Zanzibar Ali Mohamed Shein (kulia) akisalimiana na rais wa Tanzania Jakaya Kikwete wakati wa sherehe za Kikwete kuapishwa jijini Dar es Salaam tarehe 6 Novemba 2010. Zanzibar iliungana na Tanganyika bara mwaka 1964, na kuunda Tanzania. [Yasiyoshi Chiba/AFP]
Tume ilifanya mikutano 54 katika mkoa wa Mjini Magharibi wa Zanzibar kuanzia tarehe 19 Novemba hadi tarehe 18 Disemba kama sehemu ya jitihada zake za kukusanya maoni ya wananchi kuhusu katiba mypa, ambayo ilipangwa kujadiliwa na Mkutano wa Bunge mwezi Aprili 2014. Uchaguzi mkuu umepangwa kufanyika 2015.
Mikutano imekuwa ikifanyika Tanzania nzima tangu Julai, na raia kutoa maoni na malalamiko moja kwa moja kwa tume. Karibia raia 200,000 walihudhuria mikutano ya hivi karibuni huko Zanzibar, kwa mujibu wa mkuu wa Tume ya Kupitia upya Katiba Mwesiga Baregu.
Hata hivyo, licha ya kupenda kuhudhuria mikutano miongoni mwa wananchi kwa ujumla, Baregu alisema washiriki walio wengi walielewa visivyo mikutano ya kupitia katiba na kura ya maoni ya wananchi kuhusu kama serikali ya muungano iwepo au isiwepo.
"Kwa bahati mbaya, Wazanzibari walio wengi wanafikiri fursa hii ya kukusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya kuandika katiba mpya ya Tanzania ilikuwa ni fursa ya kutathmini muungano, lakini haikuwa hivyo," aliiambia Sabahi.
Visiwa vya Zanzibar viliungana na Tanganyika bara mwaka 1964 kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika mchakato huo, serikali ya Tanganyika ilivunjwa, lakini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilibakizwa kuwepo pamoja na serikali mpya ya muungano iliyoundwa.
Katika katiba ya sasa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayojitawala kwa sehemu ina mamlaka ya kisheria katika mambo ya ndani, wakati serikali ya muungano wa kitaifa inadhibiti sera ya hazina ya serikali, mambo ya nje, jeshi na ulinzi, madaraka ya dharura, uhamiaji, madeni na biashara ya taifa.
Salim Hassan Khamis, mwenye umri wa miaka 55, mzaliwa wa Zanzibar aliyehudhuria mkutano katika Jimbo la Magomeni, alisema viongozi wanapaswa kuelewa kwamba wananchi wa Zanzibar wanataka kuwa na uzito sawa wa kisiasa kama bara. "Kama ilivyo, unaposema muungano [serikali], inaeleweka kuwa serikali ya Tanganyika," aliiambia Sabahi.
Khamis alisema baadhi ya watu wanafikiri kwamba kwa sababu Zanzibar ni ndogo kuliko Tanganyika, inapaswa kunyenyekea ndani ya muungano. Lakini hiyo ni hoja isiyohitajika, alisema, kwa sababu Zanzibar ilikuwa ni taifa huru kabla ya kuungana na Tanganyika ambayo nayo ilikuwa huru.
Deus Kibamba, mwanasheria na mkurugenzi mtendaji wa Dawati la Habari za Raia Tanzania, alisema aina ya serikali iliyopo imepitwa na wakati.
Kibamba alisema viongozi katika ngazi mbalimbali za serikali hawafuati mipaka ambayo imeelezwa katika makubaliano ya muungano ambayo inaeleza wazi ni wizara zipi na sekta za viwanda zilizo katika jukumu la serikali ya muungano na ni zipi zilizoachwa kusimamiwa kipekee na serikali za ndani ya Zanzibar na bara.
Alisema kwa mfano, serikali ya muungano kwa sasa inaigharimia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambayo inahusika na bara tu na sio Zanzibar.
Alisema tatizo lilianza wakati serikali mbili zilipoungana pamoja, wakati asasi za serikali ya Tanganyika zilipoingizwa katika serikali ya muungano bila ya kufuata kanuni kuhusu mamlaka ya kisheria au kushughulikia kujirudia kwa dhima na mahitaji ya bajeti.
Kibamba alisema suluhisho linalowezekana linaweza kuhusisha kurejesha serikali ya Tanganyika na kuanzisha bunge la jamhuri ambapo waziri mkuu angewakilisha serikali ya muungano na kila nchi ingekuwa na rais wake mwenye madaraka machache.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayehusika na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa George Mkuchika alisema maoni ya raia yalikuja kwa wakati, kwa kuwa madhumuni ya tume ni kuchambua mawazo yao na kuwasilisha matokeo yake kwa taifa kwa ajili ya kujadiliwa.
Alisema mchakato wa kuandika katiba unahusisha kupiga kura ya kukubali au kupinga mawazo na kuwahamasisha Watanzania kuendelea kuzungumza wazi bila ya woga. "Jambo pekee ninaloweza kusema ni kwamba raia wote wana haki ya kutofautiana mawazo, lakini watafikia muafaka wa jinsi tunavyotaka katiba yetu iwe kupitia masanduku ya kura," aliiambia Sabahi.

No comments:

Post a Comment