Wednesday, December 5, 2012

MJI MKONGWE UNAHITAJI KUTUPIWA MACHO


Salim Said Salim Mwandishi wa habari mkongwe Zanzibar
Salim Said Salim Mwandishi wa habari mkongwe Zanzibar
MWISHONI mwa wiki sehemu ya nyuma ya jengo maarufu na la kihistoria la Beit el Ajaib (Nyumba ya Ajabu) liliopo Forodhani, Mjini Unguja, liliporomoka. Kwa bahati njema hayakutokea maafa makubwa, lakini kuanguka kwa majumba haya katika sehemu mbalimbali za Mji Mkongwe ni hasara kubwa kwa historia ya mji wa Zanzibar.
Tukio hili la kuporomoka kwa jengo la Beit el Ajaib, lililopo pembezoni mwa Ngome Kongwe iliyojengwa na watawala wa Kireno, ni kuendelea kuporomoka majengo ya zamani, baadhi yao yalijengwa takribani miaka 200 iliyopita katika Mji Mkongwe.
Jengo hili la ghorofa tatu, kila moja likiwa na urefu wa zaidi ya futi 40 ambalo linatazama na bandari ya Zanzibar, lilijengwa na Sultan Seyyid Barghash bin Said (1880-88), ni la ina yake na hakuna linalofanana nalo katika Afrika ya Mashariki.
Kwa muda mrefu sasa jengo hili maarufu duniani kote, kama yalivyo mengine mengi ya zamani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, yameonekana kuchakaa na kuhitaji matengenezo ya haraka.
Baadhi yamekuwa yakiporomoka moja baada ya jingine, hasa wakati wa mvua za masika au vuli na hata kusababisha maafa na hasara kubwa.
Kwa kweli hali iliyojitokeza ni ya kusikitisha. Hata hivyo, baadhi ya majumba haya, yamefanyiwa ukarabati mkubwa kwa misaada kutoka taasisi za Umoja wa Mataifa na nyingine za kimataifa. Miongoni mwao ni iliyokuwa nyumba ya sultani, zahanati ya jamii ya Ismalia na nyingine nyingi.
Majengo yaliyofanyiwa ukarabati sasa yanapendeza na kuwa vivutio kwa watalii, lakini toka kufanyiwa ukarabati huo zaidi ya miaka 15 iliyopita, hakuna juhudi za kuyatunza na labda yanangojewa yachakae na kutafutiwa misaada ya kuyakarabati kutoka nje.
Majumba haya ya zamani na njia nyembamba za sehemu ambazo yapo, ndiyo yaliyosababisha Mji Mkongwe wa Zanzibar kuvutia utalii na kutangazwa kama urithi wa dunia.
Lakini jambo la kusikitisha ni kuona yametupwa na serikali. Wakati umefika kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wananchi wa Visiwani kwa jumla kutambua kuwa Mji Mkongwe ni urithi unaotaka kuenziwa na kutoruhusu kupotea.
Sio vibaya kutarajia nchi za nje na mashirika ya kimataifa kusaidia kutunza majengo haya ya kihistoria, lakini ni aibu na fedheha kuona wao ndio wanaotarajiwa kuyashughulikia.
Hii ni historia ya Zanzibar na ni watu wake ndio wanaowajibika kwanza kuyatunza na wageni kusaidia tu.
Kwa muda mrefu sasa nchi yetu imebweteka kwa kutegemea misaada hata ya kutengeneza bustani au ujenzi wa vyoo vya shule. Tumejenga utamaduni wa kuona hiyo ni kazi ya wageni na sio yetu, kama vile historia ya Zanzibar haina uhusiano na watu wake.
Lazima kwa serikali na wananchi kubadilika na kuyaona majengo haya ya kale, hasa yale yenye historia ya kuvutia kama Beit el Ajaib, yanatunzwa na kushughulikiwa ipasavyo.
Kichekesho kingine ni kwamba panapotokea taasisi ya Visiwani kutafuta fedha za kukarabati majengo ya zamani, kama lilivyofanya Baraza la Biashara, wamiliki wa viwanda na wakulima kwa jumba maarufu la mvumbuzi wa kiingereza, David Livingstone, baadhi ya viongozi wa serikali huja juu kutaka majengo haya yakabidhiwe serikali.
Hivyo serikali ilikuwa wapi wakati majengo haya yalipokuwa karibu kuporomoka? Huu sio mwenendo mzuri hata kidogo na unawakatisha tamaa Wazanzibari wanaoipenda nchi yao na wenye nia njema ya kusaidia kuyatunza majengo haya ya zamani.
Mwenendo huu hauna maelezo yoyote yale isipokuwa ni kielelezo cha roho mbovu kwa baadhi ya watu waliopo madarakani.
Tuache tabia hii inayowavunja moyo wananchi kwani kuyakakarabati na kuyatumia majengo hayo haina maana kwamba wameyataifisha kwani yanabakia kuwa mali ya serikali na wao kama wananchi ni sehemu ya serikali.
Kwa sasa tunapaswa kubadilika na kuwa na mpango maalumu wa kutenga vifungu vya fedha katika bajeti zetu za matumizi ya serikali ya kila mwaka kwa ajili ya kuyahudumia majengo haya ya kihistoria tuliyorithi kutoka kwa wazazi wetu.
Tukumbuke kuwa watalii wengi na wana-historia hufika Zanzibar kuyaangalia majengo haya ya kihistoria, lakini tukiyaruhusu kuporomoka hao watalii watakuja Zanzibar kufanya nini?
Wakati umefika na kwa kweli tumechelewa, kwa serikali kuhakikisha kuwa katika bajeti yake ya matumizi ya kila mwaka panatengwa fungu maalumu la kuyashughulikia majengo ya zamani, hasa yale ya kihistoria.
Kama tunaweza kutafuta fedha kujenga majumba mapya ya wizara za serikali na kuonekana kuwepo mashindano ya kufanya hivyo, kwanini tushindwe kutafuta fedha za kuilinda historia yetu? Ni kweli haiwezekani kuyakakarabi yote kwa wakati mmoja, lakini inawezekana kuifanya kazi hii kwa uwamu.
Kinachohitajika ni kuwepo mpango mzuri badala ya sehemu kubwa ya mapato ya serikali kutumika kwa safari za viongozi zisokwisha na kujinunulia magari ya fahari kwa viongozi na watumishi wa idara na taasisi za serikali.
Haya yanafanyika huku tukijigamba kwamba ati tunafanya kila juhudi za kupunguza umasikini unaowakabili watu wetu. Huku ni kujidanganya na wananchi wanajiuliza masuala mengi na kukosa majibu.
Sio vizuri kujikita kwa mambo ya fahari na anasa na kuipa mgongo historia yetu. Vizazi vijavyo havitatusamehe kama tutayatelekeza majengo haya na kupotea na watu kubaki kuhadithia habari za majengo haya wakati yakiwa yameshatoweka. Hawatatusamehe hata kidogo kwa kushindwa kuwarithisha historia hii tuliorithi kutoka kwa wazazi waliotutangulia mbele ya haki.
Watajiuliza hawa wazee wetu walikuwa watu wa aina gani na wakati huo hatutakuwepo katika dunia hii kujitetea.
Tuchukuwe juhudi sasa ya kuhifadhi maeneo muhimu ya historia Unguja na Pemba ili historia isije kutuumbua kwa kuipoteza sehemu muhimu ya historia ya Zanzibar na watu wake.

No comments:

Post a Comment