Friday, November 30, 2012

CHANGAMOTOZINAZOIKABILI SUKZ


Changamoto za sasa zinazoikabili SUKZ


Viongozi wakuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar.
(Imechukuliwa kutoka mtandao wa kijamii wa Facebook)
Mtazamo wangu ni tafauti na wengi walionitangulia, ila turudi katika malalamiko dhidi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUKZ). Kwa jinsi hali ilivyo na mageuzi yaliyotegemewa baada ya kuundwa kwa SUKZ, tatizo kubwa lipo kutokana na kasi ndogo ya mabadiliko katika zile huduma muhimu za jamii. Na nafikiri wanasiasa watachukuwa dhima hii, kwani walipokuwa wanafanya kampeni zao, walionesha kama kwamba mabadiliko yatakuja siku moja.
Nina imani hata kama Chama cha Wananchi (CUF) kingelikuwa ndicho muundaji pekee wa serikali, basi kusingekuwa na tafauti kubwa katika kasi ya maendeleo kutokana na hali ya nchi ilivyo na ugumu wa msukumo wa gurudumu la maendeleo.
Ninaloliona mimi kwa sasa, changamoto kuu kwa SUKZ ni kusukuma kasi ya mabadiliko iendane na ahadi na matumaini waliyoyatoa wakati wa kuunda serikali.
Nafasi ngumu katika SUKZ haipo kwa CUF pekee, bali hata kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) chini ya Rais Ali Mohammed Shein kina changamoto nyingi kutoka kwa wale wahafidhina wasioutaka mfumo huu wa uundwaji wa serikali.
Ugumu kwa CCM Zanzibar ambao tumeona ukweli wao (walio wengi) hasa katika Baraza la Wawakilishi namna gani chachu ya mabadiliko inavyowasukuma katika uchangiaji wa hoja zao. Tatizo ni vitisho vya kufukuzwa au kusulubiwa kutoka kwa wachache ambao tangu mwanzoni walionekana kutokuwa tayari kuunda serikali ya mfano huu.
Sikubaliani na watu wanaposema CCM wengi hawakuutaka mfumo huu, ila kwanza na tuanze na tafsiri ya wengi ni kitu gani ikiwa asilimia 66 (kama sikosei) ya Wazanzibari, CCM na CUF, wote, waliunga mkono maridhiano na muundo wa serikali hii.
Ila nakubaliana na wingi wa walioukataa mfumo huu wakitokea CCM, bado uwingi wao huo (hata ikiwa wote ndio waliokataa) bado ni mdogo mbele ya umma ulioukubali mfumo huu.
Changamoto kubwa katika wapenda mabadiliko ndani ya CUF na CCM waliounda SUKZ kwa nguvu ya hoja na imani ya mabadiliko ni wahafidhina kutoka CCM na wale CUF waliochoka na kasi ndogo ya mabadiliko katika nchi.
Upande wa CCM wahafidhina kuona uwazi katika Baraza la Wawakilishi na umoja wa wawakilishi hao ni chungu isiyomezeka. Bado hawana njia madhubuti za kuwadhibiti wapenda mabadiliko katika CCM ambao ndio wengi walio na nafasi za chini. Nguvu za wengi hawa wapinga mageuzi kwenye CCM ni za midomo na kelele nyingi na sababu kuu ni kuchochea istifhamu za ndani ya SUKZ ili pavunjke turudi kwenye mizozano.
Kwa CUF wenye mbwembwe za kuukosoa mfumo wa SUKZ wao wana agenda yao moja pia, kuhakikisha historia ya CCM inaondoka visiwani. Hawa ndio wanaopingana na zile hekima za wakuu wa chama chao wanaohisi au wenye nia madhubuti ya kuwa na ushirikiano wa kweli na CCM wapenda mabadiliko na wenye muelekeo unaofanana.
Wengi wa kundi hili la CUF si wakaazi wa Zanzibar, na hufikira njia moja ya mambo haya kumaliza kadhia hizi ni kuingia katika mzozo wa kinguvu baina yao na wanaowaona kuwa wabishi wa mabadiliko hususan katika mfumo wa Muungano.
Ila wanasahau kwa nchi za kKafrika kushindana na dola hususan iliojaa vikosi visivyo na maadili hata za mafunzo juu yao wenyewe ni kukaribisha vifo vya watu ambavyo vinaweza kuepukwa. Hawatazami ushahidi uliopo katika nchi zilizokumbwa na majanga ya namna hii na mpaka hii leo hakuna hatua zilizochukuliwa na taasisi za nje zaidi ya kelele; na mwishowe nao wakasukumwa katika muundo wa serikali za umoja. Zimbabwe ni moja kati ya mfano mzuri. Kwa jinsi wanavyomchukia Rais Robert Mugabe na kumwachia atawale mpaka hii leo, ni vyema tukatathimini mafunzo yake.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar itafanikiwa, na itaendelea kuwepo na hatua baada ya hatua mabadiliko yatafuata. Kilichofanyika katika uchaguzi wa Bububu ni hekima za kweli baina ya vuguvugu la wanamageuzi ndani ya CUF na CCM. Kilichokusudiwa hasa hakijaonekana na kimetoweka, ni ushindi kwa vuguvugu la wanamageuzi kwa pande zote mbili.
Gurudumu linaendelea na mafunzo yapo na wapi pa kurekebiswa. Hii ni picha ya awali ya namna gani vyama vijiandee kwa uchaguzi mkuu wa 2015. Na kwa waheshimiwa wa pande zote wenye msukumo mmoja, wameziona changamoto hizi na wazifanyie kazi.
Tatizo kubwa la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kutoa matumaini makubwa yasiyoendana na hali ya ukweli wa nchi hususan kwa kuzingatia changamoto zilizopo baina ya vyama vinavyounda hii taasisi. Wakati umefika wa kuangalia mikakati mipya yenye kuweka vipaumbele kwa maendeleo ya wananchi hususan katika sekta ya afya, elimu, kilimo na ajira kwa wananchi. Mabadiliko yakianza huko, basi wepesi wa kusikilizwa na kufahamika ni rahisi.
Muungano ni suala la mabadiliko yanayotaka hekima itakayowajumuisha Wazanzibari wengi kuwa pamoja, katika kuunganisha nguvu. Ni sawa yapo baadhi ya mambo yatakayotakiwa kupatiwa muafaka ili kufikiwa lengo. Kama Muungano ulivyoundwa ukiwa na masuala machache mpaka sasa yamefika yaliyopo, basi na ufumbuzi wake unahitaji zaidi hatua hizo ziendane na wakati. Tutafika ikiwa busara na hekima zitatumika.

No comments:

Post a Comment