SMZ yazuia watu wasishuhudie kesi ya Uamsho
Viongozi saba wa Jumuiya ya Kiislamu ya
Uamsho walifikishwa katika Mahakama Kuu ya Vuga mjini Zanzibar hivi leo,
lakini chini ya ulinzi mkali wa karibuni vyombo vyote ya ulinzi na
usalama, huku wananchi wakizuiwa kabisa kukaribia hata eneo la mahakama
hiyo.
Askari wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, wakiwemo wale wa Jeshi la Kujenga la Taifa (JKU),
waliyazingira maeneo yote yanayokaribiana na jengo la Mahakama Kuu, huku
wakiwazuia watu hata kukaribia jengo hilo. Watu wengi walioachangia
maoni yao kupitia mitandao ya kijamii kuhusu namna kesi hii
inavyoendeshwa, wamesema kwamba usiri, nguvu na vitisho vya hali ya juu
vinavyooneshwa na SMZ katika muendelezo wa kesi hii, vinaashiria ukosefu
wa uadilifu, woga na kutokujiamini kwa serikali mbele ya viongozi hao
wa Uamsho iliowakamata.
“Hao (askari wa SMZ) hawana kazi za kufanya
ndio maana wameambiwa nendeni mkakusanyike alau muonekane kama mpo. Na
hiyo ni ushahidi kuwa hao Uamsho wana nguvu kuliko hao wanaoiendesha
hiyo kesi….”, yalisomeka maoni ya mchangiaji mmoja aliyejitambulisha kwa
jina la Dula Said.
Mchangiaji mwengine aliyejitambulisha kwa
jina la Rashid Abbas Machano alisema kwamba binafsi alipita karibu na
eneo la mahakama na akaona kwamba “mpaka njia ya kwendea Mnazi Mmoja
imefungwa”, akiongeza kwamba hilo halikuwa jambo la haki kwani “watu
wanahitaji kupata taarifa.”
Awaali mawakili wa viongozi hao walikuwa
wamelalamikia kuwepo kwa jaji asiyeweza kutoa dhamana kwa watuhumiwa hao
na hivyo wakawasilisha madai yao ya kubadilishiwa jaji mwenye uwezo wa
kutoa maamuzi. Itakumbukwa kwamba tangu viongozi hao walipokamatwa kwa
mara ya kwanza zaidi ya mwezi mmoja sasa, bado hawajapatiwa dhamana,
licha ya dhamana zao kuwekwa wazi, lakini kwa masharti ambayo wengi
wanaamini kwamba ni sawa na kulazimisha waendelee kubakia rumande wakati
kesi yao ikiendelea kusikilizwa.
Kutokana na maombi ya mawakili hao,
wamefanikiwa kuweza kubadilishiwa jaji ambae atakuwa na uwezo kwa
kuitolea maamuzi kesi hiyo. Lakini katika tukio la leo, Jaji huyo
aliweza tu kuwaita kwa majina yao na kisha kuahirisha tena kedi hiyo
hasi tarehe 6 Disemba 2012.
No comments:
Post a Comment